2012-12-12 08:17:08

Mapadre jiwajibisheni kutafuta na kuchuchumilia utakatifu wa maisha!


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na changamoto ya Uinjilishaji Mpya ni mwaliko kwa waamini, lakini zaidi kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, wanajibidisha kutafuta na kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kama njia ya ushuhuda makini unaopania kumtangaza Yesu Kristo Mkombozi wa dunia kwa watu wa nyakati hizi, ambao wengi wao wamemezwa na malimwengu. RealAudioMP3

Huu ni wito uliotolewa na Askofu Emmanuel Adetoyese Badejo, Mwenyekiti wa Idara ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, wakati wa mkutano wa Umoja wa Mapadre wa Majimbo Katoliki Nigeria. Anasema, utakatifu wa maisha ni nyenzo muhimu sana katika Uinjilishaji Mpya, kama ambavyo dhana hii ilivyovaliwa njuga na wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Roma.

Ushuhuda wa maisha adili na matakatifu ni chachu ya wongofu wa kweli kwa waamini ambao hawaoni tena mlango wa Kanisa kwa miaka mingi kutokana na kumezwa mno na pilika pilika za maisha ya dunia hii.

Haitoshi kwa waamini kupokea Sakramenti za Kanisa na kuonesha idadi kubwa katika vitabu vya kumbu kumbu za Kanisa, lakini jambo la muhimu ni kuhakikisha kwamba, waamini hawa katika hatua mbali mbali za majiundo yao ya Kikristo wanafahamu fika Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili waweze kusimama kidete kuiungama imani yao kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili.

Kwa kufanya hivi, waamini hao watakuwa wanaendeleza mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, changamoto kwa waamini walei katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo na mwaliko kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Katekesi ya kina na makini, iwawezeshe waamini kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia kwa njia ya Neno la Mungu; Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, Mafundisho Jamii ya Kanisa bila kusahau matendo ya huruma kwani hii ni Injili katika matendo. Uinjilishaji Mpya unalidai Kanisa kuchuchumilia daima wongofu wa ndani kama sehemu ya hija ya maisha na utume wake hapa duniani.

Uinjilishaji Mpya kama alivyosema Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa SECAM unaligusa Kanisa zima hata kwa Bara la Afrika ambalo bado linaonekana changa ikilinganishwa na Makanisa mengine Barani Ulaya.

Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni hati ambazo zina utajiri mkubwa wa vipaumbele vya Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Biblia ni Maktaba kubwa inayomwezesha mwamini kupata maisha mapya, mwaliko kwa waamini kujenga na kuimarisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vyao pamoja na kuwashirikisha wengine utajiri wa Neno la Mungu, kwani kila mwamini anachangamotishwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Askofu Badejo anasema, waamini wajifunze kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa, kama chemchemi ya utakatifu, kwanza kabisa kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa kuchunguza dhamiri na kufanya toba ya kweli. Kila Mkristo anawajibu wa kurithisha Imani, kama alivyosema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa kuzindua Mwaka wa Imani.








All the contents on this site are copyrighted ©.