2012-12-12 07:36:44

Baada ya kukaa uhamishoni, Rais wa zamani wa Madagascar ameamua kurudi nchini mwake!


Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amefanikiwa kufanya mazungumzo na Rais wa zamani wa Madagascar Marc Ravalomanana ambaye amekubari kurudi nchini kwake baada ya kuwa uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2009.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam Jumanne tarehe 11 Desemba 2012, Rais Kikwete amesema Ravalomanana amekubali pia kutokugombea katika uchanguzi utakaofanyika nchini humo mwezi Mei 2013 ili kuleta amani na utulivu.
“Nimezungumza na Rais Ravalomanana na amekubali kurudi nchini kwake madagascar na kukubali kutokukugombea uchaguzi ujao kama maamuzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) yalivyofikiwa katika vikao vyake vya hivi karibuni”, amesisitiza Rais Kikwete.
Rais kikwete amefafanua kuwa Ravalomanana anarudi nchini Madagascar bila masharti yoyote na atapewa ulinzi na Serikali ya nchi hiyo ikisaidiana na Jumuiya ya SADC.
Kwa upande wake Rais Ravalomanana amemshukuru Rais kikwete kwa kufanikisha mazungumzo hayo na amesema, anaheshimu maamuzi yaliyotolewa na SADC kwa lengo la kuisaidia Madagaska kuwa katika hali ya amani.
“Ninamshukuru Rais Kikwete kwa kufanikisha mazungumzo haya na niko tayari kurudi nchini kwangu kujenga, kuimarisha na kushirikiana na wananachi ili kuleta amani na utulivu,” amesema Ravalomanana.
Rais kikwete alipewa jukumu na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika la kufanya mazungumzo na Marais wote wa wawili, Rais wa sasa wa Madagaska Andry Rajoelina na Rais wa zamani Marc Ravalomanana ambapo mazungumzo bado yanaendelea kwa upande wa Rais Rajoelina.








All the contents on this site are copyrighted ©.