2012-12-12 08:06:09

Askofu mkuu Ruwaichi asema, unabii una heshima na madai yake!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, inapenda kukushirikisha tafakari ya kina kuhusu Unabii, kama inavyoletwa kwako na Askofu mkuu Yuda Thadeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania. RealAudioMP3

Hivi karibuni alisema, watu wanaibuka na kujipachika majina mazito yenye maana na madai yake. Wale wanaojipachika majina kama: Nabii, Mtume na Mpakwa, kwa urahisi kabisa, pengine hawaelewi undani na madai ya majina haya, bali wanatafuta heshima na nafasi zinazoendana na majina hayo. Anasema, Nabii au Mtume ni watu wanaopaswa kuheshimiwa, kusikilizwa na kuthaminiwa.

Lakini Nabii wa uongo ni mtu anayejitangaza, anayejitafuta mwenyewe na kushughulikia mno malimwengu. Nabii wa kweli ni mjumbe wa Mungu, aliyeitwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya kuyashughulikia mambo matakatifu. Unabii wa kweli ni tunu na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na unapata uhalali wake kutoka kwa Mungu mwenyewe, kwani anamjua, anamfahamu na kumtenga yule anayemtaka kwa ajili ya malengo yake, akiwa na mtazamo sahihi kuhusu wito na majukumu yake.

Askofu Mkuu Ruwaichi anasema kwamba, Mwenyezi Mungu anamwita mtu ili kuutumikia Mpango wake; kwa kuwalisha, kuwalea pamoja na kuwaangazia mwanga wake ili kutangaza Neno la Mungu, akisukumwa na Roho Mtakatifu, Roho wa Mungu. Nabii anatumwa ili kuwatangazia watu ukweli.








All the contents on this site are copyrighted ©.