Mzee Madiba bado amelazwa! Wengi wanamwombea ili apone haraka!
Mzee Nelson Mandela Rais mstaafu wa Afrika ya Kusini amelazwa kwenye Hospitali ya
Kijeshi mjini Pretoria kwa ajili ya kuchunguza afya yake na kwamba, kuruhusiwa kwake
kutoka hospitalini hapo kutategemea matokeo ya uchunguzi unaoendelea kufanywa ili
kubaini kile kinachomsumbua kwa sasa.
Hayo yamesemwa na Bi Nosiviwe Mapisa-Nqakula,
Waziri wa Ulinzi nchini Afrika ya Kusini, baada ya kumtembelea Mzee Mandela mapema
jumatatu tarehe 10 Desemba 2012. Anawaalika wananchi na watu wote wenye mapenzi mema,
kuendelea kumkumbuka Mzee Mandela katika sala zao, ili aweze kupona mapema na hatimaye,
kuendelea na maisha yake ya kawaida. Kwa sasa anahitaji utulivu na mapumziko makubwa
zaidi na hakuna sababu ya kubabaika. amekazia Bi Mapisa-Nqakula.
Wasi wasi
ulianza kutanda miongoni mwa wananchi wa Afrika ya Kusini baada ya kimya kikuu kuhusiana
na ugonjwa wa Mzee Madiba na kwamba, alikuwa anahudumiwa kwenye Hospitali ya Kijeshi.
Umaarufu wa Mzee Mandela ndio unaowafanya watu wengi kutaka kufahamu maendeleo ya
afya yake. Ni kiongozi na mfano wa kuigwa katika mapambano ya kutafuta haki msingi
za binadamu, uhuru wa kweli, amani na upatanisho.
Watu kutoka sehemu mbali
mbali za dunia wanaendelea kutuma salam na matashi mema, ili Mzee Madiba aweze kupona
haraka. Rais mstaafu Nelson Mandela ana umri wa miaka 94 tangu alipozaliwa.
Taarifa
ya Serikali iliyotolewa siku ya Jumanne tarehe 11 Desemba 2012 inaonesha kwamba, Mzee
Madiba anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na kwa sasa anaendelea vyema na tiba. Mzee
Madiba alilazwa hospitalini tangu tarehe 8 Desemba 2012.