2012-12-11 10:46:03

Hali ya amani, usalama na maendeleo Ukanda wa Sahel ni tete!


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anaonya kwamba, kinzani za kisiasa, vitendo vya kigaidi, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na silaha za megendo ni kati ya mambo yanayochangia kuhatarisha amani na usalama kwenye nchi zilizoko kwenye Ukanda wa Sahel.

Vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na majeshi ya waasi Kasikazini mwa nchi ya Mali ni hatari kubwa. Kuna watu zaidi ya millioni 18.7 wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na baa la njaa na watoto zaidi ya millioni 1 wanakabiliwa na tishio la utapiamlo wa kutisha. Tatizo la Mali linaweza kupatiwa ufumbuzi ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itajifunga kibwebwe ili kukabiliana na hali hii sanjari na kusaidia mchakato wa kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, ili kujenga na kudumisha amani na utulivu katika Ukanda wa Sahel.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo siku ya jumatatu, tarehe 10 Desemba 2012 wakati akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ukanda wa Sahel unaziunganisha nchi za: Mauritania, Niger, BUrkina Faso na Algeria ya Kusini.

Akizungumzia kuhusu hali tete iliyoko Mali, Bwana Romano Prodi, Mjumbe maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Ukanda wa Sahel, anasema, kwa sasa kuna haja ya kuharakisha kujenga umoja wa kisiasa pamoja na kuendeleza mapinduzi ya kidemokrasia yaliyokwishafikiwa nchini humo na kwamba, anaunga mkono hoja ya kupeleka majeshi ya ulinzi na usalama kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa ingawa uamuzi wa namna hii una gharama kubwa. Mkazo unapaswa kuweka katika majadiliano ya amani, ili suluhu ya kweli iweze kupatikana.

Wananchi wa Mali wanapaswa kuanza kujiandaa kushiriki katika uchaguzi mkuu ambao utafuata misingi ya ukweli, uwazi na demokrasia. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linabainisha kwamba, kuna haja ya kuwa na njia pana zaidi ili kuweza kufikia malengo ya: usalama, maendeleo na huduma za kiutu katika Ukanda wa Sahel ambao kwa sasa unakabiliwa na uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu pamoja na kukithiri kwa vitendo vya kigaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.