2012-12-11 07:23:29

Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili ni kielelezo cha imani na furaha ya kweli inayokumbatia uwepo wa Kristo katika maisha ya mwanadamu!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi jioni, tarehe 8 Desemba 2012, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili, aliungana na waamini pamoja na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali kwa ajili ya kutolea heshima Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili iliyoko kwenye Uwanja wa Spagna, mjini Roma.

Baba Mtakatifu katika tafakari yake alifanya rejea kwenye Injili ya Luka inayosimulia jinsi ambavyo Neno wa Mungu aliingia katika maisha ya mwanadamu katika hali ya ukimya na unyenyekevu mkubwa; tukio kama hili, leo hii lingepewa umuhimu wa pekee na vyombo vya habari.

Watu wana mahangaiko mengi ya maisha, hawana nafasi ya kukaa na kutulizana, ili kuweza hata kulitafajari kwa kina Neno la Mungu, lakini Bikira Maria alifanikiwa, kwani alikuwa ameungana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yake, hii ndiyo maana ya kukingiwa dhambi ya asili. Huu ni uhusiano ambao ni huru kabisa wala haufungamani na ubinafsi, kiasi kwamba, moyo wake unaambatana kabisa na moyo wa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anaukumbusha umati uliokuwa umehudhuria kwenye tukio hili kwamba, sauti ya Mungu inavuka mipaka, kinzani na vurugu za maisha zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Mpango wake unagusa undani wa mtu na katika shughuli zake za kiuchumi, kisiasa, kimaadili na kiroho. Bikira Maria ni mwaliko wa kuzamisha mpango wa Mungu katika maisha ya kila mwamini.

Wokovu wa ulimwengu anasema Baba Mtakatifu si juhudi za kisayansi, kiteknolojia au kisiasa, bali ni neema ya Mungu inayoonesha upendo wa dhati mintarafu ufunuo unaopata utimilifu wake katika Yesu Kristo. Bikira Maria amejaa neema, hali inayoonesha ukuu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu na kwamba, upendo wake unaweza kufunika ubinafsi unaoendelea kujionesha katika maisha ya mtu binafsi, kifamilia, kitaifa na kimataifa.

Zawadi ya maisha inaonekana kupoteza thamani yake na matokeo ni matumizi haramu ya dawa za kulevya. Upendo wa Mungu ndio unaoweza kuzima utupu kama huu unaojionesha katika maisha ya mwanadamu, upendo ambao unajichimbia katika neema ya Mungu.

Bikira Maria ni kielelezo cha furaha ya kweli inayopata chimbuko lake katika moyo ambao uko huru bila mawaa ya dhambi. Ukristo ni Injili ya furaha na kamwe si kikwazo kinachomkirimia mwanadamu furaha ya kweli kama wanavyodhani watu wengine ndani ya Jamii wanaoangalia tu sheria na mambo yanayokatazwa. Sheria na nidhamu ni mambo msingi kutokana na udhaifu wa mwanadamu unaopelekea madhara kwake binafsi na kwa wale wanaomzunguka. Ni changamoto ya kukataa katu katu kishawishi cha ubinafsi na kukumbatia upendo wa kweli.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, furaha ya Bikira Maria ni kamilifu kwani ndani ya moyo wake hakuna doa la dhambi ndiyo maana amekuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Akapewa dhamana na kumtunza na kumlea Mwana wa Mungu; akaanza maisha yake ya hadhara, akaendelea kumfuatilia katika imani hadi pale aliposimama chini ya Msalaba, akashuhudia ufufuko wake: Yesu ni chemchemi ya furaha ya Bikira Maria, Kanisa na kwa kila mtu.

Kipindi cha Majilio ni mwaliko wa kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu anayezungumza katika ukimya wa ndani, ili kupokea neema inayomkomboa mwamini kutoka katika lindi la dhambi na ubinafsi, ili kuonja ile furaha ya kweli.







All the contents on this site are copyrighted ©.