2012-12-10 09:20:20

Watanzania wanaoishi Roma waadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania kwa Ibada ya Misa Takatifu


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, watanzania wanaoishi na kusoma Roma, Jumapili iliyopita tarehe 9 Desemba 2012 wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kusherehekea Miaka 51 ya uhuru wa Tanzania. Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa. Ibada hii imefanyika kwenye Kanisa la Chuo cha Mtakatifu Petro, mjini Roma. RealAudioMP3

Wapendwa katika Kristo,

Tunayofuraha kukutana tena, siku hii ya leo tunapoadhimisha Jumapili ya pili ya Majilio ikiwa ni pamoja na kuadhimisha miaka 51 ya Uhuru wa Nchi yetu. Tunalo pia jambo la tatu litakalofanyika leo, yaani uchaguzi wa Viongozi wa Umoja wetu kadiri ya Katiba inayotuongoza.

Katika Jumapili hii ya pili ya Majilio, inasikika tena sauti ya nabii inayotangaza furaha iliyowajia waisraeli ambao ilibidi wakombolewe kutoka utumwani Babeli. Nabii Baruku anawatangazia waisraeli kuwa Mungu atawaongoza kwa furaha katika mwangaza wa utukufu wake, kwa ile rehema na haki itokayo kwake. Anawaalika wavue nguo za matanga na huzuni na wavae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu milele. Wajifunge nguo ya haki itokayo kwa Mungu na wajipige kilemba kichwani cha utukufu wake Aliye wa milele.

Katika Injili ya Luka tumeisikia pia Sauti ya Yohana Mbatizaji iliyokuwa inaunguruma nyikani ikiwaalika watu wafanye ubatizo wa toba liletelo ondoleo la dhambi kwa maneno aliyoyaandika Nabii Isaya akisema: “Itengenezeni njia ya Bwana Yanyosheni mapito yake…. Palipopotoka patakuwa pamenyooka, palipoparuzwa patalainishwa; na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu”.

Katika somo la pili, kama ilivyosikika Jumapili iliyopita, Paulo akiwasifia Watesalonike kwa jinsi walivyoimarika katika imani na upendo kwa Kristo, leo Paulo anawasifia waamini Wafilipi kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuineneza injili na anawaombea ili pendo lao lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; wapate kuyakabili yaliyo mema; ili wapate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali wamejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.

Ndugu zangu waamini, katika kipindi hiki cha Majilio tunaalikwa kwa namna ya pekee tuitayarishe njia ya Bwana anayekuja kutuletea furaha, haki, amani, umoja, mapatano na kila lilo jema. Ni kuiga mfano wa hao manabii kama Baruku na Yohana Mbatizaji, ni kuwa tayari kutangaza furaha inayokuja bila woga tukiambizana, kila mmoja katika nafasi yake na madaraka aliyo nayo, tuwe tayari kuishi na kutenda kadiri atakavyo Mungu.

Kutenda kama walivyofanya Wafilipi ambao Paulo amewasifia. Hapo ndipo tutakapokuwa tunashiriki nasi katika kuuleta ukombozi aliotuletea Bwana wetu Yesu Kristo, anayetangazwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Majilio, akitualika tuwe tayari kumpokea na kumpatia nafasi katika maisha yetu ili kazi yake ya ukombozi iendelee kufanyika.

Tumekutana leo pia kwa lengo la kuliombea taifa letu. Tunaposali kuliombea taifa linalofanya maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru wake, yapo mambo mawili muhimu yanayoweza kutuongoza vizuri katika maadhimisho haya: kwanza ni shukrani kwa Mungu na jambo la pili ni tafakari juu ya safari yetu kama taifa.

Sisi Watanzania tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu. Kwa kipindi hiki chote, taifa letu limeonja baraka nyingi za Mungu. Tumekuwa ni taifa lenye amani na utulivu. Tukiyainua macho yetu na kutazama nje ya mipaka yetu tunajionea wenyewe mataifa ambayo badala ya amani, umoja, mshikamano na ustawi yanaishi katika machafuko, vita na kutoaminiana. Tunazidi kumshukuru Mungu pia kwa ugunduzi wa rasilimali nyingi ambazo zinatufanya tuamini kuwa kama tutakuwa na moyo wa uzalendo, na mipango madhubuti, taifa letu linaweza kunyanyuka kutoka katika lindi la umaskini na kuhesabiwa kati ya mataifa dunia yenye kusimama vizuri.
Hata hivyo, tusingependa kujidanganya kuwa tumepiga hatua kubwa katika kuidumisha misingi hiyo tuliyoiona hapa juu, hata kama tunaweza kusema kwa dhati kabisa kuwa hali yetu si mbaya sana kama ya nchi zinazosambaratika kwa kukosa amani na umoja. Kwa hilo tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu.

Lakini tunapomshukuru Mungu kwa mema anayolijalia taifa letu, tunapaswa pia kuitafakari safari yetu ya pamoja kama taifa. Hapo juu nimesema hali yetu si mbaya sana ikilinganishwa na mataifa mengine yanayosambaratika. Kwa maneno mengine, hali yetu pia si nzuri sana, na tunapaswa kuwa makini kuiboresha ili tusiangukie katika migogoro na machafuko.

Tunapenda katika maadhimisho haya kuiombea serikali yetu na watu wake. Tunapenda kuipongeza serikali pale inapotimiza vema wajibu wake na kutambua hatua za maendeleo ya kijamii zinazopigwa na serikali yetu. Tunaona na kutambua pia jinsi serikali yetu inavyojitahidi kuweka mipango madhubuti ya maendeleo. Lakini pia tunaona jinsi ambavyo mipango mingi haitekelezwi kikamilifu.

Katika taifa letu inazidi kujengeka mifumo ya kiuchumi na kisiasa ambayo haileti matumaini ya kulifanya taifa libaki limedumu katika misingi mizuri na madhubuti iliyoanzishwa na waasisi wa taifa letu. Hali hii inalifanya taifa letu, pamoja na kuwa taifa changa, kuanza kuonesha dalili nyingi za kuchoka. Hii ni kwa sababu pale mifumo ya kiutendaji inaposhindwa kuwa sababu ya matumaini, watu huchoka. Watu wanapochoka lolote linaweza kutokea.

Katika siku za hivi karibuni yamezidi kuongezeka matukio ya ukiukwaji wa haki. Tunazidi kushuhudia hali ya raia kukaidi amri za dola na mkono wa dola ukitumia nguvu zinazopitiliza. Tunaendelea pia kushuhudia utamaduni wa kujichukulia sheria mkononi unavyozidi kujengeka katika taifa letu.

Zaidi sana matukio ya vurugu za kidini yanazidi kuongezeka, yakivuka mipaka ya kashfa za maneno dhidi ya dini nyingine na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na kutishia usalama wa taifa kwa ujumla. Vile vile pengo la wenye nacho na wasiokuwa nacho linazidi kuongezeka, na kufanya utawale utamaduni wa ubinafsi na kutokujali.

Haya na mengine mengi yanazidi kuitikisa misingi ya umoja, amani na mshikamano iliyowekwa na waasisi wa taifa letu. Katika mazingira kama haya sote tunapashwa kuwajibika na kuwa sehemu ya ufumbuzi, kwa kuirudia njia sahihi ya mshikamano wa kitaifa, ili tuzidi kulinda amani na umoja, lakini pia kusaidia kuleta ustawi kwa kila mwananchi kwa kujali maslahi ya wote (common good).

Sisi kama waamini tuliosikia leo maneno ya manabii yanayo waalika waisraeli na hivyo kutualika sisi kuzivua nguo za matanga na huzuni na kuvaa nguo za uzuri na utukufu utokao kwa Mungu milele, kutubu na kuifuata njia ya Bwana, hatuna budi kuyatazama hayo tuliyoainisha hapo juu na hasa yale ambayo yanatufanya tubaki katika nguo za matanga na huzuni na tuone ni kwa namna gani tutaweza kushiriki kuyaondoa.

Bila woga, kama alivyofanya Yohani mbatizaji, hatuna budi kuwaalika watu kufanya toba na hili ni kwa kuyakemea kwa ushujaa kabisa, hayo yanayotukosesha uhuru na maendeleo tukabaki tumefungwa kama watumwa na mbaya zaidi kufanywa watumwa na ndugu zetu na watu wetu wenyewe wasiothamini utu wetu na maendeleo ya watanzania wote.

Taifa letu pia lipo katika kipindi mahsusi cha historia yake. Tunajua kuwa sasa nchini pote unaendelea mchakato wa Katiba mpya. Lengo ni kuwa na chombo kitakachosimamia misingi ya uadilifu na uzelendo kulingana na mahitaji ya mazingira ya sasa.

Ni sala yetu kuwa Katiba mpya iwe ni zao la uadilifu na isimamie misingi ya uadilifu inayotetea na kulinda haki na hadhi ya utu wa kila mtu. Hata hivyo, hatuna budi kukumbuka kuwa Katiba isiyoheshimiwa na kuzingatiwa kwa dhati inakuwa imepokonywa uhai wake.

Tunapaswa kama taifa kujenga pia utamaduni wa kuheshimu katiba na kuzingatia taratibu zinazotuongoza. Hata katika hili tujiulize, sisi tuko wapi na tumesimama wapi katika kuchangia, hasa katika yale ambayo tunafikiri ni muhimu yakatiliwa msisitizo na yaonekane wazi katika Katiba itakayotuongoza.

Nilipokutana nanyi kwa mara ya kwanza niliwaalika tuone ni kwa namna gani nasi twaweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa marekebisho ya Katiba. Naamini viongozi wrtu, na hasa hao watakaochaguliwa, watakuwa mstari wa mbele kutuingiza katika mawasiliano na wataalamu ambao waweza kutusaidia ili nasi tuwe tayari kutoa mchango wetu.

Katika haya yote, tunaona wazi kuwa taifa letu linapaswa kuitafuta upya ile fahari ya miaka ya kwanza ya uhuru wetu, ambapo wazo lililotawala lilikuwa ni ujenzi wa taifa lililoshikamana katika nyanja zote na nyezo kuu katika ujenzi huo wa taifa ilikuwa ni moyo wa uzalendo.

Maadhimisho ya kumbukumbu ya uhuru yanapaswa kuwa ni fursa ya kutoa matumaini ya kuijenga safari yetu kuelekea lengo la ustawi wa taifa letu na kukuza moyo wa kujali maslahi ya wote.

Baba Mtakatifu Benedikto 16 katika hati yake Spe Salvi anasema: “Wakati wa sasa, hata kama ni mgumu, tunaweza kuuishi na kuukubali kama unatuelekeza kwenye lengo, kama tunaweza kuwa na hakika na lengo hilo, na kama lengo hilo ni kubwa ya kutosha kuweza kuhalalisha jitihadi ya safari” (Spe Salvi, 1).

Changamoto zinazolikabili taifa letu tuzitumie kama kichocheo cha kujirekebisha na kujizatiti katika ujenzi wa taifa. Uhuru unaotoa matumaini ni kichocheo muhimu katika kuvishinda vikwazo vinavyotaka kutuzuia tusilifikie lengo la taifa.

Utume wa Kanisa katika Tanzania na kwetu pia tulio nje ya Tanzania katika kipindi hiki ni hasa kuwasaidia watu kuutambua wajibu wanaokuwa nao kwa Mungu na kwa taifa, kama walivyofanya hao manabii, kwa kusema, kukemea, kufariji na kutia moyo kwa yale yote waliyoona ya kujenga na kufaa, na yale ambayo hayakuwa na mwelekeo wa kujenga.

Ndugu zangu, nasi tuige mfano wa hao walioamini, wakawa na upendo kwa Mungu na Kristo Mkombozi wetu na tuhakikishe kuwa yale yaliyo na thamani na yatakayo tukomboa tunayakuza na kuyaendeleza na yaliyo kinyume chake tusiyape nafasi na tuwe tayari kuyapinga na kuyakemea. Tuitengeneze njia ya Bwana na kuyanyosha mapito yake ili wote wenye mwili wauone wokovu wake.

Tumsifu Yesu Kristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.