2012-12-10 09:31:05

Utamaduni mpya wa majukumu ya watu wa ndoa na familia kuhusiana na majukumu mbali mbali ndani ya Familia


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tafakari zetu zilizotangulia zimetuhakikishia kuwa familia na kazi ni miito miwili tofauti lakini yenye asili moja na malengo mamoja yaani ustawi wa familia na jamii nzima. Japo mila na desturi hutofautiana kulingana na wakati na mahali hata hivyo nakualika leo tuendelee na tafakari yetu tukiangalia uwiano wa kazi na familia lakini tukizama zaidi kati hizi aina mbili za ndoa ambazo ziko bayana machoni pa wengi. Yaani ndoa ya kimila na ndoa kimwezi. RealAudioMP3
Katika ndoa ya kimila mwanamume anafanya kazi nje ya familia na mwanamke anafanya kazi ya nyumbani yaani kutunza nyumba na watoto. Katika ndoa hii ya kimila wana-ndoa wote wanamchango mkubwa wa familia lakini kwa namna tofauti. Ndoa za aina hii zilikuwa nyingi sana miaka ya nyuma lakini leo wengi tunakiri kuwa ndoa za aina hii zimebaki chache.
Aina ya pili ya ndoa ni hii ya kimwezi. Hapo wana-ndoa wote mume na mke wanashiriki sawa katika kazi za nje yaani katika kazi zenye kuleta ajira na mishahara na hapo hapo wanashiriki sawa katika malezi na makuzi ya watoto wao.
Kwetu Afrika ni utamaduni mpya lakini ambao umeshika kasi na tunapaswa kuupokea. Labda la msingi ni kufanyia marekebisho ila bado nafasi ya mama na baba iendelee kubaki imara katika malezi. Kwani kwa hakika nafasi ya mama haiwezi kubebwa na baba na hali kadhalika nafasi baba haiwezi kumezwa na nafasi ya mama kama waraka wa familiaris consortio wa mwenye heri Yohane Paulo II ulivyotuelekeza katika vipindi vyetu vilivyotangulia.
Ni vizuri tukumbushane kuwa namna zote mbili za kuwajibika kwenye maisha ya ndoa ni sahihi. Iwe mmoja anafanya kazi nje ya familia na mwingine anajishughulisha zaidi na familia au iwe wote wanafanya kazi za nje ya familia na hapo hapo kushiriki sawa katika makuzi ya watoto. La msingi ni kuheshimiana na kuthamini mchango wa kila mmoja katika makuzi na malezi ya familia. Na kila anayetekeza wajibu fulani autekeleze kwa upendo na faida ya familia nzima.
Ni mwaliko wa kuondokana na ile fikira potofu kuwa huyu mwenzangu ni golikipa yuko tu nyumbani hafanyi chochote anasubiri tu kupokea toka kwangu. Ufanisi wa maisha ya familia ni ushirikiano na kutiana matumaini katika nyajibu tofauti zenye lengo la kujenga familia. Maneno kama vile “Pole, asante, endelea mbele ni vikolezo muhimu katika maisha ya ndoa na familia.
Kutoka Studio za redio Vatikani ni mimi padre Raphael Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.