Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, ametoa daraja takatifu la Ushemasi
kwa Mafrateri sita waliokuwa wanasoma Seminari kuu ya Kipalapala na Peramiho na Segerea
baada ya kuhitimu sehemu hii ya kwanza ya majiundo yao ya Kipadre. Ibada hii imefanyika
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki Mbeya.
Katika
mahubiri yake, Askofu Chengula, amewataka waamini kujitosa kwa hali na mali ili kujenga
Kanisa linalowategemea sana, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari
na kumbu kumbu ya maadhimisho ya miaka 50 Jubilee ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican,
ambao unatoa mwongozo wa pekee kwa waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha
na utume wa Kanisa. Umoja na mshikamano wa dhati ni matunda ya Roho Mtakatifu kwa
Kanisa.
Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kujenga na kudumisha umoja,
upendo na mshikamano wa dhati na wachungaji wao, daima wakiwa mstari wa mbele kutolea
ushuhuda wa imani tendaji badala ya kuendekeza majungu na migawanyiko isiyokuwa na
tija wala maendeleo na ustawi kwa Kanisa. Imani hii kwa namna ya pekee, ijioneshe
kwa kuiungama, kuiadhimisha, kuiishi na kuisali. Waamini walipambe Kanisa kwa njia
ya matendo na maisha yao adili.
Mashemasi wapya ni Karolo Betold Ilonga kutoka
Seminari kuu ya Kipalapala. Shemasi Francisko Edward Ngao kutoka Seminari kuu ya
Peramiho. Shemasi Simoni Msompa kutoka Seminari kuu ya Peramiho. Shemasi Thomas
Mwampamba kutoka Seminari kuu ya Segerea. Shemasi Augustino Kanku Lukusa wa Shirika
la Marafiki wa Kristo.