Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe afariki dunia kwa ajali ya gari!
Askofu mkuu Ambrose Madtha, Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe, amefariki dunia
Jumamosi jioni tarehe 8 Desemba 2012 baada ya gari alilokuwa anasafiria kugongana
uso kwa uso nje kidogo ya Mji wa Abijan. Askofu mkuu Madtha alikuwa anarejea nyumbani
baada ya maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Dereva
wake pia amefariki katika ajali hii. Katibu wa Balozi pamoja na mtawa mmoja wamesalimika
ingawa wamepata majeraha.
Rais wa Pwani ya Pembe ametuma salam za rambi rambi
kwa Kanisa Katoliki nchini Pwani ya Pembe pamoja na kwa familia ya Marehemu Askofu
mkuu Ambrose Madtha kutokana na msiba huu mkubwa. Anasema, amepokea kwa majonzi makubwa
habari za msiba wa Askofu mkuu Ambrose Madtha.
Marehemu Askofu mkuu Madtha
alizaliwa kunako mwaka 1955 nchini India; Akapadrishwa mwaka 1982. Baada ya kutumikia
sehemu mbali mbali za Balozi za Vatican, kunako mwaka 2008, Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, alimteua kuwa Balozi mpya wa Pwani ya Pembe. Anakumbukwa na wengi
nchini humo kutokana na jitihada zake za kuhimiza majadiliano kama njia ya kumaliza
mgogoro wa kivita uliokuwa umeitikisa Pwani ya Pembe kwa miaka ya hivi karibuni.