2012-12-08 08:41:28

Wanawake Wakatoliki endeleeni kutafakari kuhusu nafasi na mchango wa Bikira Maria katika maisha yenu!


Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA kilipoanzishwa yalifungwa rasmi hivi kariuni kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, aliwataka wanawake kwa namna ya pekee kuiga mfano wa Bikira Maria aliyeonesha huruma na upendo wa pekee kwa wote wanaoteseka; mwaliko na changamoto ya kuendelea kufanya tafakari ya kina juu ya nafasi ya Bikira Maria katika maisha ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, kwani Yeye ni msaada wa daima. RealAudioMP3

Wanawake katika hija ya maisha yao anasema Askofu Padilla, wanakabiliana na changamoto mbali mbali, zikiwemo kinzani, migawanyiko, migogoro, kujilaumu na dhamiri dhaifu. Lakini wanapaswa kutambua kwamba, Mama Kanisa anawaalika kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo katika vitendo kwa njia ya kutumikia; kuwapenda wengine kwa upendo wa Kristo; nguvu wanayoweza kuipata kwa kushiriki vyema katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha hali ya juu kabisa ya upendo wa Mungu na Kristo kwa waja wake.

Waamini wanapaswa kushinda ile nguvu inayowakandamiza chini katika ubinafsi, uongo, maovu na kinzani ambazo zinawafanya kujitenga na upendo wa Mungu, kama ambavyo Baba Mtakatifu alivyowahi kuwaambia Vijana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo, Jumapili ya Matawi, kunako mwaka 2010. Msukumo wa Kimungu unamwezesha mwamini kuwa huru n hivyo kuweza kuukumbatia upendo wa Mungu. Mwamini daima ajitahidi kumwinulia Mwenyezi Mungu roho yake, kwa njia ya neema na maombezi ya Bikira Maria.

Askofu mkuu Padilla anasema kwamba, kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia inayoweza kumsaidia mwanadamu katika kuboresha maisha yake, lakini bila upendo kwa Mungu na mwanadamu, maendeleo yote haya ni bure kabisa. Mwanadamu hana budi kujivika fadhila ya unyenyekevu ambayo kimsingi ni alama ya imani inayomwilishwa pia kwa njia ya mapendo kwa jirani, kama alivyofanya Bikira Maria alipomtembelea Elizabeti, kiasi kwamba, aliweza hata kumshirikisha baraka ambazo alikuwa amekirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Unyenyekevu, utayari na uwazi wa Bikira Maria, ulimstahilisha kushiriki katika istoria ya ukombozi, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Bikira Maria ni mfano wa unyenyekevu na maisha ya sala endelevu, inayomwonesha mwamini anayejiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, hata Mwenyezi Mungu akamwinua kuliko binadamu wengine wote, kwa kumtakasa na dhambi ya asili pamoja na kumpaliza mbinguni, ili kushiriki utukufu wa Mwanaye Mpendwa.

Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kujitakatifuza ili siku moja waweze kufikia ukamilifu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Sala iwe ni kielelezo cha hamu ya kumtafuta Mwenyezi Mungu pamoja na kupania kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani.

Mwishoni Askofu mkuu Francisco Padilla anawaalika WAWATA na waamini katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanaishi vyema ahadi zao za Ubatizo, daima wakijitahidi kuwa Wakristo na raia wema; kwa kutimiza nyajibu na utume wao kwa Kanisa na kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Jamii ya watanzania wote.








All the contents on this site are copyrighted ©.