Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili "Kweli Bwana ameufunua ukombozi
wake machoni pa mataifa ameonesha haki yake"
“Atukuzwe Mungu…. Aliyetuchagua kabla ya kuumbwa ulimwengu”. Maneno haya ya mtume
Paulo, yanatufumbulia ukweli mkuu kwamba: mwanzoni kabla ya uwepo wetu, kuna uchaguzi
wa kimungu katika Kristo. Yaani, hatupo hapa ulimwengu kwa bahati nasibu, au kwa
kufumuka tu kama uyoga, au kwa msukumo fulani wa lazima. La hasha. Binadamu kabla
ya kuwepo hapa ulimwenguni tumefikiriwa, tumehitajika na tumechaguliwa na Mungu Baba
“kabla ya kuumbwa ulimwengu.”
Leo tunaadhimisha
mwanzo wa uwepo wa “Bikira Maria Immakulata”. Ina maana kwamba, uwepo wake ulifikiriwa,
uliandaliwa, na kuchaguliwa na Kristu “kabla ya kuumbwa ulimwengu”. Ndugu zangu, budi
ieleweke kwamba katika kuzaliwa hapa duniani, hakuna binadamu, anayemchagua na kumwandaa
mama yake atakakotungwa mimba na tumbo atakalozaliwa, bali anashtukia tu amezaliwa
kwa mama yeyote yule.
Mwingine unashtukia umezaliwa kwa mama mnene sana, mwingine
kwa mama mwembamba; mwingine kwa mama kichaa, kwa mama wa kabila hili, kwa mama wa
dini hii au ile kwa mama mbaya au kwa mama mwema, nk. Ni Yesu pekee aliweza kumwandaa
mama yake wa kumzaa. Akamwumba na kumtengeneza vizuri, akamkinga na dhambi na kasoro
zote. Mwumbaji anazaliwa kwa kiumbe chake. Ama kweli “Mwenye bahati habahatishi”
Ndiyo bahati na neema ya uhakika aliyopata Mama yetu Bikira Maria.
Leo kwa
imani yote kanisa linatufundisha jinsi kulivyokuwa asili au chanzo cha kukingwa dhambi
ya asili huyu mzazi mtakatifu wa Mungu. Fundisho hilo la kanisa linathibitisha vipengele
vikuu viwili: Mosi, kwamba Maria alikingiwa dhambi ya asili toka pale alipotungwa
mimba; Pili, tendo hilo la kukingiwa dhambi ya asili ni tendo la huruma na ni la pekee
sana la Mungu Baba litokanalo na mastahili ya Kristu. Yaani kutokana na Kristu tu,
ndiyo Maria ameweza kukingiwa dhambi ya asili.
Ili kulielewa tendo hilo la
ajabu la huruma na upendo wa Mungu kwa Maria kupitia kwa Yesu Kristu, tusome na kutafakari
sana somo la kwanza. Somo hilo linaeleza vizuri juu ya mapato ya dhambi ya kwanza
ya Adamu na Eva. Binadamu hao walipoteza neema ile ya utakatifu wa awali waliyopata.
Kwa hiyo, walivunja urafiki wao na Mungu wakabaki kumwogopa Mungu aliyewaumba kwa
sura na mfano wake.
Aidha umoja na uhusiano ule mzuri uliokuwapo kati ya mwanaume
na mwanamke ukakorofika na kuwa katika ukinzani. Mwanaume akaanza kujiona mtawala
wa mwanamke. Mapato ya dhambi iliyotendwa na binadamu wa kwanza haikuishia kwao tu.
Adamu na Eva walitenda dhambi zao binafsi, lakini dhambi hiyo ikatunasa sisi binadamu
wote yaani, dhambi ya kutoshiriki uzima wa Mungu, tulioshirikishwa sote ili kuwa na
umoja naye. Dhambi hiyo inatutenga na binadamu wenzetu na kutufanya tusiishi kwa amani,
kwa umoja na upendo na watu wote. Hiyo ndiyo hali yetu halisi.
Maria ni binadamu
pekee, aliyekingwa, toka mwanzoni kabisa mwa maisha yake yaani, toka pale alipotungwa
mimba hakuwa na doa lolote la dhambi. Huruma ya Baba ndiyo ilitimiliza tendo hilo
la kuteuliwa na la kukingiwa dhambi Bikira Maria. Huruma ya Baba kwa nafsi hii ya
Maria ni dhidi ya uovu unaomiliki ulimwengu, yaani, kule kumweka Maria juu ya kila
uovu na dhambi ambayo budi kila mmoja wetu apambane nayo kutokana na hali halisi ya
ubinadamu ulioanguka.
Maria alibarikiwa kwa baraka zote za kiroho kwa njia
ya mwanae Kristo. “Nitaweka uadui kati yako na mwanamke”: maneno haya yanatimia kwa
Maria. Toka alipotungwa mimba, amekuwa adui binafsi wa Shetani. Maria ni mpinzani
wa shetani kwa vile hakuna uhusiano wala ushirikiano wowote katika kuujenga ufalme
wa uovu. Maria ni mpambanaji wa kwanza dhidi ya dhambi.
Imani ya kanisa inatufundisha
ukweli mwingine kuhusu mwanzo huu wa Maria, na kuhusu uteuzi huu wa pekee unaomkinga
Maria na kila kosa na kumbariki kwa baraka zote na sadaka ya Kristu msalabani. Hili
ndilo fumbo kuu kwetu tunaloweza kuliona leo ni kwamba kila adhimisho la kikristu,
adhimisho la ukuu wa kazi ya ukombozi ya Kristo; ni neema ya msingi, ni neema safi
na ya fahari kuu. Yaani, katika nafsi ya Maria, ukuu wa kifo na ufufuko wa Kristo
unatukuka zaidi na unapata umuhimu wa pekee.
Mwenyeheri John Henri Newman
anasema kwamba katika Maria, “Bwana amefunua ukombozi wake, machoni pa watu wake ameonyesha
haki yake. Amemtendea Maria zaidi ya kile alichokifanya kwa binadamu wengine. Kwa
wengine amewapa neema na uweza wa kuendelea kuanzia pale walipoanza kuishi hapa duniani:
Kumbe kwa Maria alimpatia neema hiyo tangu mwanzo kabisa.” [J.H. Newman].
Ukweli
huo unatoa mwanga kwenye usiku wa giza la fumbo la kibinadamu kwa hoja mbili: Kwa
upande mmoja, katika Maria, sisi tunaweza kutambua siyo nani ni kipeo cha binadamu,
bali tunatambua nani ni binadamu halisi. Yaani tunatambua hali halisi aliyokuwa nayo
binadamu toka mwanzo kabisa mwa maisha yake, siyo suala la kidhahania (kimawazo tu)
ambalo yabidi kulifuata, bali ni kitu halisi ambacho kinafanya uwepo wetu binafsi,
na kinacholenga kwenye kuwa waana warithi kwa njia ya Yesu Kristu kadiri ya mapenzi
ya Baba. Nje ya ukweli huu unaopinga mahusiano hayo na Kristu ni uwongo.
Kwa
upande mwingine, kutokana na fumbo tunaloadhimisha leo, tunaweza kujitafiti kikamilifu
maovu yetu ya kiroho na maovu yanayotawala ulimwenguni kutokana na dhambi ya asili.
Ukweli wa dhambi ya asili ni ukweli ambao ni mgumu sana kuupokea, lakini kukataa au
kusahau uwepo wa dhambi ya asili ndiyo unaofanya hali halisi ya kibinadamu kuonekana
kuwa fumbo lisilotanzulika.
Kutotambua na kudharau kwamba hali halisi ya ubinadamu
wetu ni tete, imejeruhiwa na ina mwelekeo wa kutenda uovu (unaosababishwa) au unaotokana
na makosa ya kielimu, ya siasa, ya kijamii, ya kitamaduni, ya kidini nk. Mama wa Mungu,
zaidi ya mtu mwingine yeyote, aliishi mang’amuzi ya fumbo hilo la ukombozi wa kibinadamu.
Katika maingilio ya adhimisho hili kubwa la fahari tunatambulishwa fumbo hilo
kwa wimbo usemao:
“Tota pulchra es Maria – U mzuri kabisa
Ee Maria.” Kwa mara nyingine tena tunapenda kukuangalia wewe, Ee Maria, ili
kutafakari uzuri wa nafsi yako: Uzuri ambao unang’ara ukweli wa ubinadamu wewe. Katika
wewe, sisi leo tunatekelezewa mradi wa Mungu ndani ya kila mmoja wetu. Mvuto unaoishi
wewe, umetokana na ukweli kwamba mioyo yetu inaona ndani yako kutekelezwa kikamilifu
matakwa na nia zako za uhalisia wa maisha.
Ubora wa ukombozi wa Kristu, ambao
unadhihirika katika mng’aro kamili ndani yako, unadhihirika na kuonekana ndani ya
historia ya kila siku ya maisha yetu. Inadhihirika katika utakatifu wa maisha ya watu
wengi wanaoishi maisha yao ya sakramenti mbalimbali hususani sakramenti ya ndoa.
Yanadhihirika
kwa wahitaji tunaoishi nao kila siku. Unadhihirika ndani ya watu wengi wake kwa waume
wanaojitolea kila dakika kuwafundisha watoto na vijana katika familia zetu na mashuleni.
Katika uaminifu na shujaa wa mapadre katika huduma za uchungaji. Huu ndiyo mwanga
unaoangaza mahali maisha yetu na kila mahali tuishipo. Tusisahau pia kwamba, mwanga
huo umezungukwa pia na giza; yaani mambo mengi yanayoukandamiza moyo pindi tunatafakari
uzuri wake. Kwa mfano, hali ya watu kukosa kazi ni usiku unaotisha kwa wengi.
Wahusika
wanawazibia wengine njia huru za ubunifu wa kiuchumi, badala ya kuwaacha watu huru
kubuni njia zifaazo. Aidha, ni jambo la kutia huruma kwa vijana ambao waliokata tama
kwa vile maisha yao yameharibika. Vijana wanaoonekana wakizurura mabarabarani, mitaani,
vijiweni; au vijana wale ambao wamefilisika kiroho na ni watupu kabisa kwa sababu
wamenyimwa haki yao ya msingi kabisa: yaani elimu. Yaani, kuelimishwa na wazazi wao,
au na watu wakubwa, au ni vijana wanaopotoshwa na wengine, hivi wanashindwa kupambanua
kati ya chema na kibaya, kizuri na kichukivu.
“Tunaukimbilia ulinzi wako,
Ee mzazi mtakatifu wa mungu, Usikatae maombi yetu katika shida
zetu, Bali utuokoe siku zote katika kila hatari, Ee Bikira mtukufu
na mwenye baraka. Ee Malkia wetu, Ee Mshenga wetu, Ee
Mwombezi wetu, Utupatanishe na mwanao, Utupendekeze kwa mwanao, Utukaribishe
kwa mwanao, Ee Bikira mtukufu na mwenye baraka. Amina.”
Tafakari
hii imeandaliwa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.