2012-12-08 12:06:59

Papa apokea "Papamobile" kwa ajili ya shughuli za kichungaji


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa tarehe 7 Desemba 2012 amepokea gari jipya aina ya Mercedes Benz kwa ajili ya matumizi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni gari ambalo limetengezwa maalum ili kumwezesha Baba Mtakatifu kuwa karibu na watu wanaotaka kumwona wakati wa hija zake za kichungaji sehemu mbali mbali za dunia; kwa kuzingatia pia viwango vya usalama na utulivu.

Kwa mara ya kwanza gari hili linaanza kutumika wakati Baba Mtakatifu atakapokwenda kuweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili iliyoko kwenye Uwanja wa Spagna, mjini Roma. Gari hili ni fupi ikilinganishwa na magari mengine ya kipapa yaliyotangulia ili kutoa nafasi ya kuweza kubebwa kwenye ndege bila usumbufu mkubwa wakati wa hija za kichungaji zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbali mbali za dunia.

Kampuni ya Mercedes Benz kwa zaidi ya miaka themanini imekuwa ikitoa magari maalum yanayotumiwa na Mapapa mjini Roma na wakati wa hija zao za kichungaji. Kwa mara ya kwanza Mercedes Benz ilitoa gari kwa Vatican kunako mwaka 1930 na ufunguo wake akakabidhiwa Baba Mtakatifu Pio wa kumi na moja.

Akielezea kuhusu gari la Papa, kama linavyojulikana na wengi kuwa "Papamobile", Bwana Alberto Gaspari mratibu wa hija za kichungaji za Khalifa wa Mtakatifu Petro anabaianisha kwamba, kwa mara ya kwanza, neno "Papamobile" lilianza kutumiwa na wananchi wa Uingereza kunako mwaka 1982; mwaka mmoja tu baada ya jaribio la kutaka kumuua liliposhindikana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tangu wakati huo, makampuni yaliyokuwa yanatengeneza magari kwa ajili ya matumizi ya Papa yalipaswa kuzingatia pamoja na mambo mengine usalama wake. Uingereza na Hispania ni kati ya nchi za kwanza kabisa kutengeneza magari kwa viwango na sifa zilizokuwa zinahitajika, ili kupunguza gharama za kumsafirisha Baba Mtakatifu, magari maalum yakawa yametengenezwa na kusafirishwa pale yanapohitajika. Baadhi ya magari haya yako kwenye Jumba la Makumbusho ya Vatican, ukifika mjini Vatican, usikose kwenda kuchungulia.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wote huu ameendelea kutumia gari lililoachwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili. Gari jipya linakidhi viwango na sifa zinazohitajika.







All the contents on this site are copyrighted ©.