2012-12-08 14:45:52

Mshikamano wa Papa Benedikto XVI kwa wananchi wa Ufillipini waliokumbwa na tufani!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi tarehe 8 Desemba 2012, aliyaelekeza mawazo yake nchini Ufilippini, akionesha uwepo wake wa karibu kwa watu waliokumbwa na tufani kubwa ambayo imesababisha maafa makubwa na watu wengi kwa sasa wamelazimika kuyakimbia makazi kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Imani na Upendo wa kidugu utakuwa ni nyenzo na nguvu ya kuweza kupambana vyema na majaribu haya. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuikimbia dhambi na nafasi zake, ili kutunza ile neema ya utakaso waliyoipokea wakati walipobatizwa. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni kielelezo makini cha ushirikiano wa neema ya Mungu.

Taarifa zinabainisha kwamba, kuna zaidi ya watu laki moja na sitini ambao hawana mahali pa kuishi na kwamba, nyumba zaidi ya elfu moja na mia tatu sitini zimehabiwa vibaya na hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Baba Mtakatifu mwishoni, amewabariki wanachama wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Italia ambao wamerudia tena ahadi yao ya kutaka kujikita zaidi na zaidi katika utakatifu kwa kushirikiana na viongozi na walezi wao kwa ajili ya azma ya Uinjilishaji Mpya.

Amewakumbuka wafanyakazi wa sekta ya afya wanaotekeleza wajibu wao katika Hospitali za Kanisa ambao kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu baada ya ruzuku iliyokuwa inatolewa kwenye hospitali hizi kufutwa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Ni matumaini yake kwamba, wahusika wataweza kupata suluhu ya kudumu kuhusiana na tatizo hili.







All the contents on this site are copyrighted ©.