2012-12-07 08:02:12

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya II ya Kipindi cha Majilio


Tunaendelea na tafakari ya Neno la Mungu, leo ni Dominika ya II ya Kipindi cha Majilio Mwaka C, ambapo Neno la Mungu latualika kukazia maisha ya toba, kusafisha njia ya mioyo yetu, maandalizi pekee kwa ujio wa Masiha. RealAudioMP3

Toka kitabu cha Nabii Baruku, Nabii anawaalika Wana wa Israeli waachane na nguo za matanga na huzuni kwa maana karibu mkuu wa furaha yu karibu. Wako Babeli katika mateso na sasa wanaalikwa kwa tumaini kubwa kwamba watarudi nyumbani. Kwa jinsi hiyo wanatakiwa kuvaa utukufu utokao kwa Mungu milele, nguo ya haki, kilemba cha utukufu kwa maana Mungu ataifanya Yerusalemu kuwa mwangaza kwa mataifa yote, na hivi toka mashariki na magharibi wana wa Yerusalemu watakusanyika kwa furaha kwa maana Mungu amewakumbuka na kuwaondolea teso lao lililotoka kwa maadui wao. Kwa sababu ya ujio wa nuru milima na mabonde vitasawazishwa ili Israeli aende salama katika utukufu wa Mungu anaporudi nyumbani.

Mpendwa msikilizaji wa tafakari Neno la Mungu, kuondolewa katika mateso kwa Waisraeli ni kielelezo cha kuondolewa na kukombolewa kwetu toka katika utumwa wa dhambi. Mwaliko kwetu ni kuacha maisha ya kale na kuingia katika maisha mapya, maisha ya kumpendeza Mungu. Tunaalikwa kukua katika imani thabiti iliyojaa ushuhuda kama tunavyoalikwa na Baba Mtakatifu Benedicto 16 katika mwaka huu wa Imani kuwa imani hukua kama inashuhudiwa kama mangamuzi ya upendo na inapohubiriwa kama mangamuzi ya neema za Mungu.

Mpendwa kuingia katika furaha ambayo Nabii Baruku anatufundisha ni kujikuza katika kusimamia Imani uliyoipokea wakati wa ubatizo ambayo yadai kukuzwa kwa njia ya Neno la Mungu na maadhimisho mengine ya Kilitrujia. Furaha na kukua katika imani lazima pia kukazia maisha hadharani na umoja wa Kanisa yanayoongozwa na imani thabiti.

Somo la Injili lataka kukazia maandalizi ya njia ya Bwana ili aweze kupita kwa usalama. Njia ya Bwana kwa hakika ni maandalizi ya mioyo yetu kwa kuishi maisha ya upendo kwa Mungu na kwa jirani. Ni kumwongokea Mungu na kuacha miungu isiyoweza kuokoa, ni kubadilisha maisha ya kale na kuingia maisha yanayoongozwa na Mkombozi pekee wa ulimwengu katika fumbo la Pasaka ambapo Mungu anaonesha upendo usiopimika.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anaponukuu Mtakatifu Paulo anapowaandikia Warumi Rom. 6:4 anatupa tumaini akisema ikiwa Kristu alikufa na kufufuka, nasi twaweza kusafiri katika njia ya maisha mapya, maisha ya kuambatana na Mungu kwa njia ya Sakramenti na Neno lake.

Maaskofu wakiwa wameunganika na Baba Mtakatifu katika Sinodi juu ya uinjilishaji kina na mpya wanataka kukazia namna ya kufunua furaha ya Kimungu, na kujenga uchangamfu na hamu mpya katika kufundisha na kuishi imani namna ya kugundua upendo wa Mungu. Basi Yohane Mbatizaji anapolia na kutangaza matengenezo ya njia ya Bwana katika Injili anataka kuamsha uchangamfu na hamu ya kila mmoja wetu kumwongokea Mungu. Nabii anataka kukazia maisha ya toba, maisha ya kuzama kwa undani katika mioyo yetu na kugungua nini tufanye ili kuishi pendo la Mungu litujialo kwa njia ya Masiha!


Mtume Paulo anapowaandikia Wafilipi anakazia ukuu wa Mungu kwamba kile kinachoanzishwa na Mungu daima huendelea kuwa mikononi mwake, kumbe hatupaswi kuwa na mashaka bali tumaini lililojaa uhakika wa Kimungu. Ili kutunza haya yote anawaomba Wafilipi wazidi kubaki katika pendo la Mungu daima, wakiongozwa na hekima itokayo juu inayoongoza mema. Msisitizo unawekwa pia katika toba yaani kukaa katika moyo safi uliojazwa matunda ya haki.

Mpendwa msikilizaji wa kipindi tafakari, nikutakie maandalizi mema ya kumpokea Masiha na zaidi sana ukizidi kukua katika imani tendaji inayojidhirisha katika mapendo kwa Mungu na jirani Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.