Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili 8 Desemba 2012
Mpendwa mwanatafakari wa Neno la Mungu, tukiwa bado katika safari ya hija ya wokovu,
maandalizi ya roho zetu kumpokea Emanueli mwana wa Mungu, Mama Kanisa haachi kutuwekea
zawadi kichocheo cha imani na furaha ya mioyo yetu. Zawadi hii ni fumbo la kukingiwa
dhambi ya asili Mama Bikira Maria, Mama wa Mungu.
Mpendwa, wote
twajua kabisa kuwa, kwa njia ya Adamu tumeingia duniani, na katika hali ya kawaida
twajua kuwa roho ikiungana na mwili lazima ipate madhara ya mwili na hivi kwa jambo
hili dhambi ya asili. Je inawezekanaje Mama huyu asipate dhambi hii? Swali hili limekuwa
likiulizwa tangu karne za kwanza za kanisa mpaka hivi leo. Mama Kanisa akisali sana
na kujikabidhi mbele ya Mungu akitazama Neno la Mungu na Mapokeo anaweka wazi ufunuo
wa Mungu mwenyewe akifundisha ulio ukweli wa ufunuo na kutangaza kuwa Bikira Maria
ni Imakulata.
Mama huyu anakingiwa dhambi ya asili kwa sababu lazima awe makao
stahili ya Mwana wa Mungu aliye mtakatifu, asiye na doa la dhambi. Ndiyo kusema kwa
vile Mwana wa Mungu ni mtakatifu asingeweza kuingia mahali pasipo patakatifu. Kumbe
kukingiwa dhambi ya asili kwa Mama Bikira Maria ni zawadi ya Kristo mwenyewe kwa mama
yake, na anaitoa zawadi hii mapema kwa mastahili ya msalaba atakaoupokea baadaye.
Mpendwa,
wazazi wetu wa kwanza walidanganywa na nyoka, wakaanguka katika dhambi ya kwanza,
wakapoteza utakatifu. Kukingiwa dhambi ya asili kwa Bikira Maria ni alama ya nguvu
ya Mungu juu ya dhambi iliyowaangusha wazazi hawa. Kumbe kwa fundisho hili la imani
tunaamini na kupata tumaini jipya kuwa kwa kuungana na Kristu, dhambi na mwovu vitapatilizwa.
Mama
Kanisa anasherehekea sherehe hii kila tarehe 8 mwezi wa kumi na mbili kila mwaka.
Sherehe haitukuzi tu usafi na utakatifu wa Mama bali ni fundisho la imani ambalo twapaswa
kuliamini kina. Fundisho hili lilitangazwa na Baba Mtakatifu Pio IX mnamo tarehe 8
Desemba mwaka 1854 kuwa FUNDISHO LA IMANI.
Mama Kanisa anaposherehekea
sherehe hii anataka kila mmoja wetu akumbuke mwanzo wa ukombozi wetu. Mama huyu alikingiwa
dhambi ili aruhusu Mwana wa Mungu kutungwa mimba katika mji usio na doa na hivi nasi
katika utakatifu huo tunaweza kukombolewa. Kwa hakika hatuwezi kukombolewa na awaye
yote aliyeguswa na doa la dhambi bali tunakombolewa na asiyeguswa na doa la dhambi
naye ni Kristu Mwana wa Mungu.
Mama Bikira Maria alizaliwa kama ambavyo Mungu
alikuwa amekusudia mwanadamu awe tangu mwanzo. Fikiria juu ya Adamu na Eva kabla ya
kutenda dhambi yao ya kwanza, walikuwa watakatifu na wakaharibu utakatifu wao kwa
kiburi na tamaa ya ulimwengu. Kinyume nao Mama Maria anatunza utakatifu aliokabidhiwa
katika neema ya Mungu. Anakuwa tunda la kwanza la ukombozi. Anakuwa tabernakulo ya
kwanza kumbeba Mwana wa Mungu.
Mpendwa, kwa sherehe hii si tu tunakumbuka mwanzo
wa ukombozi wetu bali pia mwisho wa maisha yetu. Ndiyo kusema tunamwomba Mama atuombee
tuweze nasi kuonja matunda ya kazi ya mwanae, tuweze kuishi bila dhambi tukilenga
daima maisha ya utakatifu. Mama huyu ni mfano wa maisha bora, ni taa ambayo inaendelea
kuwaka anapojitokeza tena na tena katika maeneo mbalimbali akileta ujumbe wa mwanae
kwa mataifa.
Ombi kwako mwana wa Mungu, ebu jaribu kufanya safari ya hija
katika maeneo mbalimbali ambayo Mama Kanisa ameyaratibisha ukaonje mapendo ya mama
huyu. Baadhi ya maeneo hayo ni Lourdes - Ufaransa, Fatima-Ureno, Pompei, Loreto-Italia
na Nyakijoga Bukoba Tanzania.
Mpendwa tukiendelea kusali kwa kujitayarisha
kwa ajili ya majilio, tunawaombea wale wote waitwao Imakulata wakashike vema utauwa
wao, wakamwite Mama Maria Bikira akawaimarishe katika utumishi wao kwa umma na kwa
Kanisa. Tunawaombea Masista wote wanaotimiza miaka 25, 50 ya utawa, wanaoweka nadhiri
za muda na za milele wakaimarishwe na Mama Bikira Maria Msaada wa Daima. Tunaziombea
Parokia zote na mashirika yote ya kitawa waliojiweka chini ya ulinzi wa Mama Bikira
Mkingiwa wa dhambi ya asili wakaimarike na kuwa safina ya umoja, upendo na ustawi
wa kiroho na hasa katika maisha ya sakramenti.
Tumsifu Yesu Kristo na Bikira
Maria.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.