2012-12-07 14:54:13

Sehemu ya kwanza ya Mahubiri kwa Baba Mtakatifu na Wasaidizi wake: Umuhimu wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita pamoja na wasaidizi wake wa karibu, Ijumaa tarehe, 7 Desemba 2012 wamefanya tafakari ya kwanza ya kipindi cha Majilio iliyoongozwa na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa ambaye amezungumzia juu ya Mwaka wa Imani, mintarafu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki kama chombo makini kitakachowawezesha waamini kuishi na kuadhimisha kikamilifu Mwaka wa Imani, kwani huu ni muhtasari wa Mafundisho Makuu na Imani ya Kanisa.

Ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaifahamu Imani yao ili kuleta furaha ya ndani, vinginevyo, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki itabaki imehifadhiwa kwenye Maktaba bila ya kuwa na manufaa makubwa katika maisha ya waamini. NI mwaliko wa kuisoma, kuitafakari na kuimwilisha katika ushuhuda wa maisha kama kielelezo cha Imani wanayoungama, Adhimisha, Ishi na Kusali. Kiini cha Katekisimu hii ni Yesu Kristo anayeendelea kuandama na Kanisa lake, kwa njia ya Maandiko Matakatifu na Mapokeo hai ya Kanisa.

Kwa njia ya Yesu Kristo anasema Padre Cantalamessa, waamini wapate fursa ya kukutana na Mwenyezi Mungu aliyejifunua katika Agano la Kale na hatima yake ni katika Agano Jipya. Ni mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini na Wayahudi, kama wanavyohimiza Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Mama Kanisa anatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayojikita kwa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Ili waamini waweze kuiungama vyema Imani yao kwa Kristo, kuna haja ya kuwa na majiundo endelevu, kama walivyofanya Mitume kwa Kanisa la Mwanzo. Hizi ni jitihada za kuunganisha mwanga wa maisha ya mwanadamu na yale ya Kimungu, kama inavyojidhihirisha pia katika Injili, Kanuni ya Imani na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.

Familia ya Mungu inawajibu wa kutangaza Kweli za Kiinjili, kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kuimarisha Imani dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa katika Uinjilishaji Mpya kwa kutafuta mbinu na nyenzo mintarafu mazingira na watu wanaoishi katika ulimwengu wa utandawazi.

Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki iwe ni nyenzo kwa ajili ya majiundo makini ya Imani kwa kutambua maudhui, madai na utekelezaji wake unaojionesha katika Imani tendaji. Ni mwelekeo mpya wa Imani unaohitaji toba na wongofu wa ndani. Baada ya kupokea zawadi ya Imani, mwamini anatakiwa kuikuza Imani hiyo ili iweze kufikia utimilifu katika maisha ya Kikristo, kwani Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni kumbu kumbu hai na endelevu juu ya tafakari ya kina kuhusu Imani thabiti wanayopaswa kuiungama na kuitolea ushuhuda amini wafuasi wote wa Kristo.

Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara wamempokea Roho Mtakatifu, Mwaliku wa kweli anayewafundisha Ukweli Wote kama wanavyosema Mababa wa Kanisa, tayari kuutolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha, kwani wamelifahamu na kuamini katika pendo la Mungu na kwa njia hii, wamemwamini Yesu Kristo kuwa ni Mtakatifu wa Mungu, mwaliko wa kujenga na kuimarisha uhusiano wao pamoja naye.

Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Neno wa Mungu alifanyika mwili akakaa kati ya watu wake, atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Waamini wakifahamu undani wa Imani yao wataweza kuiungamana na kumtolea ushuhuda Yesu Kristo na huu ndio mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Waamini wafahamu kwa dhati kabisa kweli za Kiinjili ili kuziungama kwa furaha kubwa.

Kristo ni Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu kwake Bikira Maria akawa mwanadamu. Kutokana na ukweli huu, Bikira Maria ni kielelezo cha kila Mwinjilishaji na Katekisita. Ni mwaliko wa kumpokea Kristo, ili kumtoa pia kwa ajili ya wengine. Waamini wakumbuke kwamba, wamempokea pia Roho Mtakatifu, kumbe wanadhamana ya kumtangaza Kristo kwa ujasiri mkubwa zaidi; wana heri wale wanaoamini katika Kipindi hiki cha Neema, kama alivyofanya Bikira Maria.







All the contents on this site are copyrighted ©.