2012-12-07 08:22:26

Nia za Jumla na Kimissionari za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Desemba 2012


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika nia zake za jumla kwa Mwezi Desemba 2012, anawalika waamini kuungana naye kwa ajili ya kuombea wahamiaji, ili waweze kupokelewa kwa moyo wa ukarimu na upendo wa dhati hususan na Jumuiya za Kikristo sehemu mbali mbali za dunia. RealAudioMP3

Anakumbusha kwamba, Maria na Yosefu walilazimika kusafiri kutoka Nazareti hadi mjini Bethlehemu ili kushiriki katika zoezi la sensa. Kwa vile kulikuwa hakuna malazi kwa ajili yao, Bikira Maria akajifungua Mtoto wake, Mwana wa Mungu katika Pango la kulishia wanyama.

Kutokana na wivu wa Mfalme Herode aliyetaka kumfutilia mbali Mfalme wa Wayahudi aliyekuwa amezaliwa punde tu!, Familia Takatifu ikalazimika kukimbilia uhamishoni Misri, ambako walikaa hadi pale hali ilipotulia. Yesu aliyaanza maisha yake hapa duniani kama Mkimbizi na Mhamiaji.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, pengine simulizi hii imekuwa ni ya kawaida mno kwa watu wengi kiasi kwamba, wanaweza kupuuzia shida na mateso wanayopata wahamiaji. Wakati huu Mama Kanisa anapotafakari kuhusu Fumbo la Ujio wa kwanza wa Neno wa Mungu; basi, waamini na watu wenye mapenzi mema wakumbuke shida na mateso wanayokumbana nayo wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kundi hili la watu lisionekane kana kwamba, ni tatizo, bali watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kama watu wengine, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao.

Baba Mtakatifu anasema, kuna mamillioni ya watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa kutokana na kukimbia madhulumu, vita na kinzani ambazo zinahatarisha usalama wa maisha yao. Watu hawa wanapaswa kueleweka na kukaribishwa kwa moyo wa ukarimu, wakiheshimiwa na kuthaminiwa. Jumuiya za Kikristo zinawajibu wa pekee kabisa kuhakikisha kuwa, zinawasaidia wakimbizi na familia zao kwa njia ya sala, mshikamano na upendo wa Kikristo. Kuna haja ya kuwa na mwelekeo na sera mpya: kiuchumi na kijamii kwa kulinda na kuheshimu utu wa kila mwanadamu; familia pamoja na kuwasaidia kupata makazi bora, fursa za kazi na huduma za kijamii.

Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, maneno haya ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, yatasaidia kulitafutia ufumbuzi tatizo la wakimbizi na wahamiaji kwa njia ya upendo na mshikamano wa kweli, kwani kila jambo linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu.


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika nia zake za kimissionari kwa mwezi Desemba 2012, anawaalika waamini kutafakari kwa kina kuhusu Kristo, Mwanga wa Mataifa, ili aweze kujifunua kwa wote, kwa njia ya ule mwanga unaoangaza kutoka mjini Bethelehemu na kuakisiwa kwenye Kanisa. Mwanga huu ulijionesha kwa mara ya kwanza yapata miaka elfu mbili iliyopita mjini Bethelemu. Huyu ndiye Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, Mwanga unaofukuza giza la dhambi katika maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anabainisha kuwa, Yesu katika ubinadamu wake ni sura ya Mungu na Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo ni sura ya Yesu ulimwenguni. Yesu anaonekana duniani wakati huu kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Kwa kuungana na Kristo, Mwanga wa Mataifa, maisha ya waamini yanakuwa ni chanzo cha mwanga wa mataifa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwamba, Mwanga wa Kristo utaweza kufukuza giza kwa wale wanaotembea na kuishi katika uvuli wa mauti; umaskini, ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na vita. Anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuruhusu mwanga huu, ili uweze kuangaza na kuleta joto katika familia; utulivu na matumaini mijini; ulete amani duniani.

Uso wa Kristo mwingi wa huruma na mapendo uwajaze furaha na kuwawezesha kuwa kweli ni wajumbe wa matendo makuu ya Mungu katika maisha yao.








All the contents on this site are copyrighted ©.