Monsinyo Georg Gànwein, Katibu muhtasi wa Papa ateuliwa kuwa Askofu mkuu
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemteua Monsinyo Georg Gànswein, Katibu
muhtasi wake, kuwa Askofu mkuu na Mkuu wa Nyumba ya Kipapa. Askofu mkuu mteule Ganswein
alizaliwa tarehe 30 Julai 1956 nchini Ujerumani. Baada ya masomo na majiundo yake
ya Kikasisi alipadrishwa kunako tarehe 31 Mei 1984.
Kunako mwaka 1993 alijiendeleza
kwa masomo ya juu na hatimaye akajipatia shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha
Kikatoliki cha Munich, Ujerumani. Kwa miaka kadhaa alifanya kazi kama Hakimu wa Mahakama
ya Jimbo pamoja na kuwa msaidizi binafsi wa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Freiburg im
Breisgau.
Kunako mwaka 1995 alianza kufanya utume wake mjini Vatican katika
Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Kanisa. Mwaka 1996 akahamishiwa kwenye Baraza
la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na huko alikuwa ni katibu muhtsasi wa Mwenyekiti
wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, akamteua Monsinyo Georg Gànswein kuwa katibu
wake muhtasi.