2012-12-05 08:20:09

Waamini bado wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutekeleza wajibu wao wa Kuinjilisha!


Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu " Uinjilishaji Mpya kwa ajili ya kutangaza Imani ya Kikristo". Mkutano huu umefanyika wakati ambapo Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Wajumbe wa Sekretarieti kuu walipata fursa ya kutafakari kwa kina kuhusu dhamana ambayo Kristo amelikabidhi Kanisa kwenda ulimwenguni kote ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu; hii ni changamoto endelevu kama alivyobainisha Askofu mkuu Nikola Etrovic, Katibu mkuu wa Sinodi ya Maaskofu.

Wajumbe baada ya majadiliano na upembuzi yakinifu, waliangalia kwa pamoja Mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi kwa ajili ya kufanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa kuandika Waraka wake baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya.

Kanisa bado linaendelea kuchangamotishwa kutekeleza dhamana yake ya Kimissionari katika Ulimwengu mamboleo, unaogubikwa na ubanifasi, ukanimungu na watu kupenda na hatimaye kumezwa mno na malimwengu. Kanisa halina budi Kuinjilisha kwa ari na kasi mpya zaidi kwa kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kutafuta lugha na njia mpya, lakini zaidi kwa kuwa na mashahidi amini wa Injili, ili kurithisha Imani kwa vijana wa kizazi kipya.

Hii ni dhamana shirikishi inayotekelezwa kuanzia ndani ya Familia, Parokia, Vyama vya Kitume, Majimbo hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Jukumu kubwa ni kuendelea kutumia fursa mbali mbali kwa ajili ya kurithisha Imani; kwa njia utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, Maisha ya Kisakramenti, Liturujia na Utakatifu wa maisha. Kanisa linatekeleza wajibu huu kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene, kwani watu wote wanapaswa kusikiliza Habari Njema ya Wokovu.

Wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya wanatarajiwa kukutana tena hapo tarehe 23 hadi tarehe 24 Januari 2013 hapa mjini Roma.







All the contents on this site are copyrighted ©.