Ujumbe wa Kipindi cha Majilio kutoka kwa Askofu mkuu Rowan Williams
Askofu mkuu Rowan Williams wa Kanisa kuu la Cantebury ambaye ni Kiongozi mkuu wa Jumuiya
ya Waanglikani Duniani katika ujumbe wake Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2012 anawaalika
waamini wa Kanisa Anglikani kugundua na kuthamini utambulisho wao kama Familia kubwa
wanamoshirikishana matumaini na kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu wanawajibika kwa ajili
ya mafao ya wengine.
Jumuiya ya Waangalikani yenye waamini wapatao millioni
themanini na kwamba, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwakirimia Kiongozi mwingine
Askofu Justin Welby wa Jimbo la Durham atakayemrithi. Anawaalika waamini kumsindikiza
kwa njia ya Sala wakati huu anapojiandaa kuanza kutekeleza utume wake hapo mwakani.
Anakazia umoja na mshikamano miongoni mwa waamini kwa kutambua kwamba, majadiliano
ya kitaalimungu yanatishia kuleta mpasuko mkubwa miongoni mwa Waamini wa Kanisa Anglikani.
Anawataka
kuonesha ushuhuda thabiti na endelevu wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, heshima
miongoni mwao na kwa viongozi waliopewa dhamana. Umoja miongoni mwa waamini wa Kanisa
Anglikani umekumbatana na kinzani na hali ya kutoeleweka hadi leo hii, lakini wanayo
bahati ya kuuona utukufu wa Mungu unaojidhihirisha kwa njia ya uso wa Yesu katika
medani mbali mbali za maisha. Lengo liwe ni kuimarisha umoja na mshikamano ili kutekeleza
utume wa Kanisa.
Kipindi cha Majilio, iwe ni fursa kuimarisha Injili ya Upendo;
Umoja na Mshikamano kati ya waamini wa Kanisa Anglikani katika Majimbo mbali mbali
duniani, hata kama bado kuna maswali kadhaa ambayo hayajapata majibu muafaka kuhusiana
na Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kwa pamoja washikamane ili kukabiliana na changamoto
zilizopo kwa sasa. Utengano isiwe ni sababu ya kuvuruga ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Waamini
washikamane katika Uinjilishaji Mpya; katika utoaji wa huduma kwenye sekta ya afya;
kusimama kidete kulinda na kutetea utu na haki msingi za binadamu, bila kusahau kuhifadhi
mazingira. Ni rahisi mno kuweza kuiona sura ya Kristo, lakini ukweli ni kwamba, waamini
wasipokuwa makini, itawawia vigumu kuweza kupata suluhu ya matatizo na changamoto
wanazokabiliana nazo. Mshikamano wa upendo pamoja na kuaminiana unaweza kuleta mabadiliko
yanayokusudiwa.