2012-12-05 07:13:13

Mwaka wa Imani: Toleeni ushuhuda halisi wa imani yenu kwa Kristo na Kanisa lake!


Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, limewaandikia waamini barua ya kichungaji inayowaalika kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba, wanaishi kikamilifu Ukristo wao mintarafu Imani ya kweli.

Barua hii ya kichungaji imesomwa rasmi tarehe 2 Desemba 2012, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, kama kipindi kilichokubaliwa na Mama Kanisa, kwa waamini kuweza kuishi vyema imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni siku maalum ambayo imetengwa pia na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kwa ajili ya kuombea amani kwenye Eneo la Maziwa Makuu.

Mwaka wa Imani kadiri ya malengo ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ni kwa ajili ya kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumbu kumbu ya miaka ishirini tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipochapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja na kuendeleza juhudi za Uinjilishaji Mpya changamoto endelevu iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican.

Maaskofu wanawaalika waamini wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuimwilisha Imani yao katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku: kwa kuisafisha, kuiungama, kuishuhudia, ili hatimaye, waweze kuimarisha maisha yao ya kiroho kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuchuchumilia utakatifu wa maisha, wito na mwaliko kwa kila mwamini.

Barua ya Maaskofu imegawanyika katika sehemu kuu tatu: sura ya kwanza inapembua kwa kina na maana juu ya Imani ya Kikristo; sura ya pili inagusia matatizo, kinzani na changamoto wanazokabiliana nazo waamini katika hija yao ya maisha ya kiroho. Sehemu ya tatu: inatoa maelekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na waamini wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Rwanda.

Kwa Wakristo, Imani ni fadhila ya kimungu inayomwezesha mwamini kupokea zawadi ya imani inayomwezesha kumuungama Mungu mmoja. Huu ni mwaliko kwa waamini kujibidisha kuifahamu Imani ya Kanisa kama inavyojionesha kwenye Kanuni ya Imani na kufafanuliwa vyema kabisa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Huu ni muhtsari wa Imani ambayo imefunuliwa na Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Kwa kuifahamu fika Imani hii, waamini wataweza sasa kuimwilisha katika vipaumbele na katika medani mbali mbali za maisha, wakitambua dhamana na wito wao kama Wakristo katika maisha na utume wa Kanisa.

Maaskofu wanabainisha kwamba, kuna matatizo, changamoto na kinzani nyingi zinazoendelea kujionesha kwa namna ya pekee dhidi ya Imani ya Kanisa Katoliki. Moja ya matatizo haya ni tabia ya ukanimungu inayojitokeza kwa namna ya pekee, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia; ustawi na maendeleo ya kiuchumi, ambamo baadhi ya wachumi wanadhani kwamba, wanaweza kufanya yote pasi na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kuna sera na mikakati ambayo inafanywa makusudi kabisa ili kuliangamiza Kanisa na Mafundisho yake: kwa kupandikiza sera za utamaduni wa kifo, zinazodhalilisha ut una heshima ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ikumbukwe kwamba, maisha ya mwanadamu ni zawadi takatifu inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Kuna sera zinazosigana kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; ndoa inayojengeka katika uhusiano thabiti kati ya bwana na bibi na wala si ndoa ya watu wa jinsia moja.

Hizi ni dalili za kumong’onyoka kwa maadili na utu wema, watu wanadhani kwamba, wanaweza kuwa na uhuru usiokuwa na mipaka, uhuru unaotaka kumng’oa Mungu katika maisha adili na utu wema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda, linawaalika waamini kuimarisha Imani yao kwa kushiriki mara kwa mara katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; kuzipokea kwa moyo wa ibada, uchaji na ushiriki mkamilifu. Jubilee ya Miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, iwe ni fursa kwa waamini kuweza kujichotea utajiri uliomo kwa kuzisoma, kuzitafakari na kuwashirikisha wengine.

Ni changamoto kwa waamini kujitahidi kuishi kikamilifu Imani yao wakianzia kwanza kabisa katika familia zao, maeneo ya kazi na sehemu nyingine za hadhara, daima wakitafuta mafao ya wengi, wakisimama kidete kulinda na kutetea haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Wajitahidi kuondokana na mambo yanayoleta chokochoko kiasi cha kuamsha hisia za chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Watambue kwamba, ukabila ni sumu ya maendeleo endelevu.

Mwaka wa Imani uwawezeshe waamini kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kikabila. Mwishoni, wanawaalika waamini kujitengea muda wa kufanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabau ya Bikira Maria wa Kibeho.








All the contents on this site are copyrighted ©.