Kanisa Barani Amerika linakusanyika Mjini Vatican kwa Kongamano litakalopembua kuhusu:
Mwaka wa Imani, Uinjilishaji Mpya na Changamoto zilizopo!
Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini, Jumanne tarehe
4 Desemba 2012 ameongoza jopo la viongozi waandamizi kutoka Vatican, ili kuelezea
juu ya Kongamano la Kimataifa litakalofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 9 hadi
12 Desemba 2012 ili kuzungumzia hali ya Kanisa Barani Amerika katika kipindi cha miaka
kumi na mitano iliyopita, baada ya maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Kanisa la Amerika
ya Kusini, iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako mwaka 1997.
Kongamano
hili linaongozwa na kauli mbiu "Kukutana na Yesu Kristo aliye hai: njia ya wongofu,
umoja na mshikamano Barani Amerika." Katika kipindi cha miaka kumi na mitano iliyopita,
Kanisa nchini Marekani, Canada na Amerika ya Kusini, limeendelea kukabiliana na changamoto
mbali mbali katika maisha na utume wake. Tema ya wahamiaji imeendelea kuwa tete katika
majadiliano na wanasiasa; mtandao wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya
pamoja na sera zinazotumika kudhibiti biashara hii ni kati ya mada tete zitakazojadiliwa
na wajumbe kwenye Kongamano hili.
Kardinali Marc Ouellet anasema kwamba, katika
kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya jinai,
kinzani, migogoro, vurugu na fujo zinazofanywa na kundi kubwa la vijana wasiokuwa
na ajira. Taasisi ya Familia imeendelea kukabiliana na kinzani pamoja na utamaduni
wa kifo unaotishia Injili ya Uhai; uhuru wa kidini, umaskini na hali ya kukata tamaa
ni kati ya mambo yanayohatarisha misingi ya haki, amani na utulivu.
Wajumbe
wanatarajiwa kujadili matatizo na changamoto zote hizi katika mwanga wa Utume wa Kanisa,
ili kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano baina ya Makanisa mahalia, wakitambua
kwamba, kwa pamoja wanaunda Kanisa la Kiulimwengu. Ndiyo maana Kongamano hili linafanyika
mjini Vatican, kielelezo cha umoja na mshikamano wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, mchungaji
mkuu.
Professa Guzman Carriquiry Lecour anasema kwamba, jumla ya wajumbe mia
mbili wanatarajiwa kushiriki katika Kongamano hili. Baadhi yao ni kutoka kwenye Mabaraza
ya Kipapa, Makardinali, Maaskofu wakuu, wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume
pamoja na wawakilishi wa waamini walei. Ni kongamano ambalo litawahusisha Mabalozi
mbali mbali kutoka katika Barani Amerika.
Jumapili tarehe 9 Desemba, 2012
Wajumbe wa Kongamano watafungua kwa Ibada ya Misa Takatifu, itakayoadhimishwa kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican na baadaye Baba Mtakatifu Benedikto wa
kumi na sita, atawasalimia na kuwapatia ujumbe wake wa kitume, chachu ya kufanyia
kazi wakati wa Kongamano hili.
Kongamano hili litafungwa pia kwa Ibada ya Misa
Takatifu, tarehe 12 Desemba 2012, Kanisa litakapokuwa linafanya Kumbu kumbu ya Bikira
Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika. Ni Ibada itakayowashirikisha waamini wengi
kutoka Amerika. Juhudi zote hizi ni katika mwendelezo wa mchakato wa maadhimisho ya
Mwaka wa Imani na juhudi za Uinjilishaji Mpya; dhamana inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa
katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.
Dr. Carl Anderson, Kiongozi
mkuu wa Knights of Columbus, anakazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Uinjilishaji
Barani Amerika; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ari na uchangamfu mkubwa zaidi,
jukumu ambalo waamini walei wanapaswa kulivalia njuga, kwa kushirikiana na viongozi
mbali mbali wa Kanisa. Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na utamadunisho, kwa kuhakikisha
kwamba, Injili ya Kristo inaota mizizi katika maisha na vipaumbele vya waamini. Bikira
Maria wa Guadalupe, awasaidie waamini kumwendea Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo.