2012-12-04 14:10:11

Uwepo wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwenye mtandao wa Twitter, mwendo ni mdundo!


Zaidi ya watu laki nne tayari wamekwishajiandikisha katika akaunti ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwenye mtandao wa kijamii wa twitter katika lugha saba, tangu ulipozinduliwa siku ya Jumatatu tarehe 3 Desemba 2012 , ingawa Baba Mtakatifu atuzindua rasmi kwa kujibu maswali wanayoendelea kumuuliza hapo tarehe 12 Desemba 2012.

Hii inaonesha kwamba, Jukwaa la Mitandao ya Kijamii lilikuwa na hamu na kiu ya kutaka kuwasiliana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, pamoja na wasaidizi wake wa karibu, moja kwa moja, mahali walipo; jambo linalowezeshwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano, ili kugusa akili, nyoyo na matamanio ya watu wanaoogelea katika mitandao hii.

Ni maneno ya Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati alipokuwa anajibu maswali kuhusu mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuanza kutumia mitandao ya kijamii kama njia ya kujenga na kudumisha majadiliano ya kina kuhusu imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu anawachagamotisha Wakristo kujitoa kimasomaso kuliinjilisha Jukwaa la Watumiaji wa Mitandao ya Kijamii.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu alikwisha onja mafanikio ya matumizi ya mitandao ya kijamii wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika mjini Sydney, vijana wengi walikuwa wanamtumia ujumbe mfupi wa maneno na kwamba, uwepo wake kwenye mitandao ya kijamii, anapania kuwafikia watu wengi zaidi.

Ni mwaliko pia kwa viongozi wengine wa Kanisa kuiga mfano huu kadiri ya uwezo wao. Kanisa halina budi kuendeleza utambulisho wake kwamba, ni Jumuiya Kubwa yenye dhamana na wajibu wa kuwasiliana na watu wengi zaidi; kujibu matarajio na matamanio ya watu wa ulimwengu wa sayansi na teknolojia mintarafu Habari Njema ya Wokovu na Kweli za Kiinjili.

Vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, kwa miaka kadhaa sasa vinaendelea kutumia mitandao mbali mbali ili kufikisha ujumbe wake kwa hadhira inayokusudiwa, kama njia ya kujenga na kuendeleza majadiliano na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mawasiliano haya kama ambavyo Baba Mtakatifu Benedikto alivyobainisha alipotembelea kwa mara ya kwanza Radio Vatican ni kutaka kujenga jukwaa la majadiliano ya kina, kwa kuunda na kuimarisha familia inayowasiliana.

Padre Federico Lombardi anasema, maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano yana matatizo na changamoto zake, Kanisa halina budi kuendelea kujifunza ili kuboresha ujumbe unaotolewa kwenye mitandao hii.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika umri wake anajifunza kutumia mitandao ya kijamii ni changamoto na mwaliko kwa Kanisa kujifunga kibwebwe ili kuonesha uwepo wake endelevu na wenye mguso katika Jukwaa la Mitandao ya Kijamii. Wasaidizi wake katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu ambao wamekabidhiwa kwao wanachangamotishwa kuiga mfano huu kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa katika majadiliano ya kina.







All the contents on this site are copyrighted ©.