Unaweza kutwitter na Baba Mtakatifu kwa anuani ifuatayo: @pontifex
Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii,
Jumatatu, tarehe 3 Desemba 2012 ameongoza ujumbe wa wakuu wa idara mbali mbali za
mawasiliano mjini Vatican katika uzinduzi wa matumizi ya Twitter kwa ajili ya Baba
Mtakatifu benedikto wa kumi na sita; mtandao wa kijamii ambao utaanza kutumiza rasmi
hapo tarehe 12 Desemba 2012, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira
Maria wa Guadalupe.
Kuanzia sasa unaweza kutweet na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita kwa kwa lugha nane: Kiingereza, Kihispania, Kiitaliani, Kijerumani,
Kipolandi, Kiarabu na Kifaransa kwa kutumia anuani ifuatayo @pontifex.
Baba
Mtakatifu anatarajiwa kuzindua rasmi matumizi haya kwa kujibu maswali kadhaa kuhusu
Imani yatakayokuwa yameulizwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni njia
muafaka anasema baba Mtakatifu kwa Kanisa kufanya majadiliano ya kina na waamini wanaoishi
katika ulimwengu wa mtandao ambao wanaonesha kiu na njaa ya kutaka kukutana na Mwenyezi
Mungu.
Itakumbukwa kwamba, tangu mwaka 2009, Vatican ilianza pia kutumia
mtandao wa Youtube na Baba Mtakatifu mwenyewe akaonesha umuhimu wa Kanisa kuviinjilisha
vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa kuvisaidia kupata tunu msingi za maisha ya kijamii
na kiutu, ambazo zitatumiwa na wahusika katika kuboresha maisha yao.
Mwaka
2010, Baba Mtakatifu akawaalika Viongozi wa Kanisa na kwa namna ya pekee, Mapadre
kushirikisha Neno la Mungu kwa njia ya mtandao, ili kuendeleza dhamana ya Mama Kanisa
katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kutumia pia maendeleo ya sayansi na teknolojia
ya habari. Mitandao ya Kijamii inaendelea kuboresha maisha ya watu wengi licha ya
changamoto na vikwazo vinavyojitokeza; lakini hata hapa Mama Kanisa lazima aendeleze
utume wake wa Kuinjilisha.
Hili ni jukwaa la majadiliano ya kina kati ya Kanisa
na watumiaji wa mitandao kuhusiana na Injili ya Kristo pamoja na Mafundisho Jamii
ya Kanisa. Baba Mtakatifu anataka kuonesha njia ya kujadiliana na watu, kwa kutambua
kwamba, Kanisa ni Mama anayesikiliza na kujali shida na mahangaiko ya watoto wake.
Hii ni changamoto pia kwa viongozi wengine wa Kanisa kujiwekea utaratibu wa kuweza
kujibu kiu na njaa ya watu katika hija ya maisha yao ya kiroho.
Uwepo wa Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika mtandao wa kijamii ni kuwakilisha sauti
ya mshikamano na viongozi wengine wa Kanisa. Ni mwaliko na changamoto kwa waamini
pia kupaza sauti zao, kwa kuwashirikisha wengine utajiri wa Habari Njema ya Wokovu
kwa njia ya majadiliano ya kina yanayogusa undani wa Imani, Matumaini na Mapenda,
fadhila za Kimungu.
Mwanzoni mwa Mwezi Desemba, watumiaji wa mtandao wanaweza
kuanza kumuuliza maswali Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita na majibu ya maswali
haya yatatolewa wakati wa kuzindua rasmi mtandao wa twitter. Mwanzoni mwa matumizi
ya mtandao huu, kutakuwa na mfumo wa maswali na majibu, kama kielelezo cha Mama Kanisa
anayesikiliza na kujali wasi wasi na matumaini ya watoto wake.