2012-12-04 10:49:40

FIDES linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 85 ya huduma ya Mawasiliano ya Kimissionari Duniani


Shirika la Habari za Kimissionari, FIDES, linaadhimisha Jubilee ya miaka 80 tangu lilipoanzishwa chini ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika mkutano wake mkuu uliofanyika kunako mwezi Aprili 1927. Lengo la FIDES ni kuhakikisha kwamba, Watu wa Mungu wanaufahamu utume na maisha ya Kanisa kwa njia ya vyombo vya upashanaji habari.

Wanashirikishwa katika kuhamasisha ari na moyo wa kimissionari kwa hali na mali; pamoja na kuendelea kuombea miito ya kimissionari, ili kazi ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu iweze kusonga mbele kwa ari kubwa zaidi. Shirika hili lilianzishwa mara tu baada ya maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Francis Xsavier, Msimamizi wa shughuli za kimissionari ndani ya Kanisa.

Kwa mara ya kwanza habari za FIDES zilianza kutolewa kwa lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kipolandi. Baada ya muda si mrefu habari zikaanza pia kuchapishwa kwa lugha ya Kiitalia kunako mwaka 1929, Kihispania mwaka 1930, Kijerumani mwaka 1932. Baada ya kukua na kupanuka kwa teknolojia ya habari hasa kwa matumizi ya mitandao, toleo la habari kwa lugha ya Kichina lilianza kutoka kunako mwaka 1998, Kireno mwaka 2002 na Kiarabu mwaka 2008.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican wanabainisha kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuendelea kujikita katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa kutumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari. Kwa mwelekeo kama huu, kuna haja kwa Mama Kanisa kuendeleza vyombo vya habari ili Injili iweze kuwafikia watu wengi zaidi.








All the contents on this site are copyrighted ©.