2012-12-03 15:09:16

Washeni moto wa mapendo kwa Kristo, Kanisa, Adhimisho la Ekaristi Takatifu ili kuzima kiu na njaa ya watu wenu!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu, tarehe 3 Desemba 2012 amekutana na Jumuiya cha Chuo Kikuu cha Mwenyeheri Beda, kilichoko mjini Roma, maalum kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka Uingereza. Anasema, anaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili Chuo hiki kiendelee kuwa ni kitalu cha miito mitakatifu kwa ajili ya Upadre na Maisha ya Kitawa.

Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa Katoliki nchini Uingereza ambalo limetoa Wamissionari wengi kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia, kama ilivyokuwa kwa Papa Gregori mkuu aliyemtuma Mtakatifu Augustine wa Cantebury kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini Uingereza. Matokeo ya kazi hii kubwa yanajionesha kwa namna ya pekee katika kipindi cha miaka mia sita na hamsini ya Imani na Ushuhuda uliooneshwa na waamini mbali mbali nchini humo.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini nchini Uingereza kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwasha moto wa imani kwa bidii na umakini mkubwa, ili Kristo aendelee kufahamika zaidi na zaidi, kwa njia ya ushuhuda wa yale ambayo wameyasikia kutoka kwa Mitume.

Watakatifu mbali mbali wameendelea kuwaonesha waamini upendo wenye mvuto unaowaelekeza wengine kwa Kristo ili waweze kumfahamu zaidi, huo ukawa ni mwanzo wa kuenea Habari Njema Uingereza, Canada na katika nchi za Scandinavia.

Kuna watu waliomwaga damu yao kwa ajili ya Kristo, ili aweze kufahamika na kupendwa, changamoto kwa Wanajumuiya hii kusali daima, kujenga utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Kusikiliza kwa makini Neno la Mungu; daima wakiwa tayari kutolea ushuhuda wa Imani yao kama walivyokuwa wafuasi wa Kristo, kwa njia ya maisha na utume wa Kipadre, kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Yesu amewachagua kama marafiki zake, changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza katika utekelezaji wa kazi ya Ukombozi sanjari na Uinjilishaji Mpya.

Baba Mtakatifu anawaalika Wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Mwenyeheri Beda kuwasha ndimi za moto zinazoleta mabadiliko katika maisha ya watu, kama inavyojionesha kwenye Agano la Kale na pale Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume siku ile ya Pentekoste. Mwanga huu uwe ni nguvu ya upendo wa Mungu unaosafisha Jumuiya au Taifa husika.

Moto huo uwashe mapendo kwa Kristo, Kanisa na Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuzima kiu na njaa ya maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, wanaweza kushibishwa kwa kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo. Ni mwaliko wa kuwatangazia ukweli wa Kiinjili kwa njia ya mapendo; wakiwaonesha Kristo ambaye ni Mkate wa Uzima wa milele. Mwanga wa Kristo uoneshe utakatifu wa maisha yao, kwa kuendelea kufuata nyayo za watakatifu kutoka Uingereza waliotolea ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa gharama ya maisha yao; mwaliko kwa kila mmoja wao pia kutamani utakatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.