Wanandoa jengeni uwiano mzuri kati ya kazi na familia!
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tunapoendelea na tafakari yetu kuhusu miito ya
familia na kazi ni vizuri leo tukumbushane kuwa miito hii miwili tofauti haipaswi
kufarakana bali kujenga mahusiano mazuri. Jambo la kushangaza
ni kuwa katika jamii yetu leo miito hii miwili iko kwenye mivutano sana na mara nyingi
familia inaonekana sio muhimu kama kazi. Wengi wanajiuliza je ni sawa kubali mshahara
kidogo ili nipokee wajibu wa uzazi au malezi ya watoto au afadhali kuahirisha uzazi
na malezi nijiendeleze na kufanya kazi zaidi ili nipate mshahara mkubwa? Lile lililo
jukumu msingi la familia yaani uzazi na malezi mahali pengi kwa sasa linahesabika
kama kazi isiyo na ujira (Unpaid work) Leo hii kazi inaonekana ndio wito pekee
wenye thamani kubwa kuliko familia. Na jambo la ajabu zaidi ni pale kazi inapomgeuza
mwanadamu kuwa chombo cha uzalishaji tu bila hata kujali utu wake. Kazi imegeuka kuwa
bidhaa tena bidhaa adimu. Hata mwanamke ambaye umama wake hauwezi kubadilishwa na
chochote leo hii wimbi la wakati linamkuta katika kudai haki sawa katika mishahara
na ajiri. Haki sawa ni jambo jema lakini nafasi ya umama katika malezi haiwezi kuzibwa
na mtu mwingine yeyote. Mahali pengine familia imehesabika na kuonekana kama taasisi
binafsi kama vile dini ambayo ni kwa ajili ya watu wachache na sio kwa jamii nzima.
Ndugu msikilizaji kazi kama ilivyo familia inamhusu kila mwanadamu aliyeumbwa kwa
sura na mfano wa Mungu haina dini wala kabila. Mwaliko wa kanisa kwa wakati wote
ni kujenga uwiano mzuri kati kati ya familia na kazi. Ni lazima tutambue kuwa japo
kazi na familia ni miito miwili tofauti lakini yote hutusaidia kudhihirisha upendo
na kukua katika utakatifu. Ni Mungu huyo huyo aliyetoa amri ya kuzaa na kuongezeka
yaani kujenga familia lakini ni huyo huyo anayempa mwanadamu amri ya kufanya kazi.
(Mwanzo 1:27-28). Kilele chake ni pale Mungu anapokubali umwilisho katika familia
nakuifanya kazi kwa wakati wote mpaka pale juu msalabani. Ndugu msikilizaji, katika
tafakari zetu toka waraka wa mwenye heri Yohane Paulo II (Familiaris Consortio) tulisema
mwanamume ni mume kwa mkewe na baba kwa watoto wake, hivyo endapo kazi za kiuchumi
zitamtenga na majukumu haya ya kifamilia basi familia yake iko hatarini. Tulisema
mwanamke ni mke kwa mumewe, lakini, mama kwa watoto wake hivyo endapo kazi zake za
kiuchumi zinamtenga na wajibu huu basi familia yake iko hatarini. Tumalizie tafakari
yetu ya leo kwa kurudia kuwa kinachotakiwa ni uwiano mzuri kati ya kazi na familia
kwani yote ni muhimu na yanategemeana. Daima tukumbuke kuwa kazi chimbuko lake ni
familia na kazi ni kwa ajili ya familia. Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi
ni Padre Raphael Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo
Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.