2012-12-03 08:03:26

Wanafunzi wa Roma wana mshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwapatia changamoto katika hija ya maisha yao ya kiroho!


Rosi Miscini kutoka Chuo Kikuu cha Roma Tre, ndiye aliyepewa dhamana ya kutoa salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya Masifu ya Jioni, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, tarehe Mosi, Desemba 2012. Hili ni tukio ambalo litaendelea kubakiza chapa ya kudumu katika hija ya maisha yao ya kiroho, kwani wamepata fursa ya kuweza kukutana na kiongozi anayewaelekeza na kuwafahamisha kwamba, Yesu yuko pamoja nao!

Wanafunzi walikabidhi Sanamu ya Bikira Maria Kikao cha Hekima ambayo imetembezwa kwenye taasisi na vyuo vikuu mjini Roma, tangu tarehe 10 Novemba, wanafunzi hao walipofanya hija ya kichungaji mjini Assisi. Sanamu hiyo imechukuliwa na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Belo Horizonte, nchini Brazil, mji ambao utakuwa ni mwenyeji wa mkutano wa wanafunzi kutoka vyuo vikuu, utakaofanyika mwezi Julai, 2013 ukifuatiwa na maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani, itakayoongozwa na kauli mbiu “iweni na furaha katika Bwana”.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni mwaliko kwa wanafunzi kugundua imani kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa kila mwanafunzi kutumia fursa hii kuweza kukutana na yesu Kristo Mfufuka. Wanafunzi wanashukuru kwamba, katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, taasisi za elimu na vyuo vikuu mjini Roma, vimebahatika kupata viongozi wa maisha ya kiroho, hali ambayo imewawezesha kushinda: woga, wasi wasi, vikwazo na ukosefu wa usalama.

Kikanisa ni mahali pao pa kukimbilia katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Urafiki ni zawadi ambayo imeendelea kuchipua miongoni mwa wanafunzi kwa njia ya imani, kiasi hata cha kuthubutu kumfungulia Kristo malango ya miyo yao. Wanafunzi wanamwomba Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aendelee kuwakumbuka katika sala zake, bila kuisahau Italia ambayo kwa sasa inakabiliwa na hali ngumu ya maisha.








All the contents on this site are copyrighted ©.