2012-12-03 15:03:08

Ujumbe kwa Siku ya Walemavu Duniani


Kila Mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Walemavu Kimataifa, kwa kukazia haki zao msingi. Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la wahudumu wa Sekta ya Afya anasema katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya kwamba, hawa ni watu wenye thamani kubwa katika maisha ya kiimani, kwani wanashiriki katika mateso na upendo wa Kristo kwa waja wake.

Utu na heshima yao vinapaswa kulindwa na kuheshimiwa; walemavu kwa upande wao, wapokee hali yao ya maisha kwa imani na matumaini. Wasikilizwe katika shida na mahangaiko yao ya ndani; washirikishwe katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwamegea ukarimu na kulinda haki zao msingi. Wapewe huduma za tiba; miundo mbinu iwazeshe kuishi kwa ukamilifu zaidi, wakiendelea kusaidiwa na Familia zao; daima mafao yao kama binadamu yapewe kipaumbele cha kwanza.

Mama Kanisa anapenda kuonesha ukaribu wake kwa watu wenye ulemavu, kwa kuwashirikisha mwanga wa Imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa kweli. Walemavu ni watu wanaopaswa kupewa tiba, lakini zaidi waonjeshwe upendo, watambuliwe, waheshimiwe na kushirikishwa katika maisha ya jamii inayowazunguka.

Wasionekane kuwa ni kikwazo na kizingiti cha maendeleo ya binadamu, kwani ni kielelezo makini cha Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Ni walimu wa upendo unaookoa na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu ya upendo, mshikamano na ukarimu mintarafu mwanga wa Kristo.

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, watu wenye ulemavu wajengewe pia uwezo wa kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji Mpya, kwa kustahimilia mateso na mahangaiko yao ya ndani pamoja na kuwatendea vyema. Imani thabiti inamwezesha mwamini kuweza kuyapokea mateso na mahangaiko yake kwa uvumilivu, matumaini na mapendo.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anapenda kuwahakikishia watu wenye ulemavu kwamba, Kanisa liko pamoja nao katika shida na mahangaiko yao ya ndani na kamwe haliwezi kuwaacha pweke! Linasubiri kuona kwamba, hata wao wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, awasaidie waamini kutambua na kuonja ubinadamu uliojeruhiwa, ili kuwapokea na kuwasaidia kutambua kwamba, hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa na yesu Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.