Uelewa sahihi wa binadamu unapata chimbuko lake katika ufunuo na akili inayobainisha
haki na wajibu wa binadamu
Baraza la Kipapa la Haki na Amani limefanya mkutano wake wa mwaka wakati huu Mama
Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani, Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatican pamoja na Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya. Bado muda kidogo
Waraka wa Papa Yohane wa Ishirini na tatu: Amani Duniani, Pacem In Terris utakuwa
unatimiza pia miaka 50 tangu ulipochapishwa. Yote haya ni matukio muhimu sana kwa
maisha na utume wa Kanisa.
Mafundisho Jamii ya Kanisa ni sehemu muafaka ya
dhamana ya Uinjilishaji inayotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia
na ni chombo muhimu sana cha Uinjilishaji katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya
Ukristo. Ni mwaliko kwa waamini kumpokea Yesu Kristo pamoja na kuendelea kumshuhudia
katika medani mbali mbali za maisha; daima wakiwa na mwono sahihi wa binadamu, utu,
uhuru na uwezo wake wa kufikiri. Ni mwono wenye mwelekeo katika maisha ya binadamu
pamoja na kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi anayostahili.
Ni sehemu ya hotuba
ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyoitoa Jumatatu tarehe 3 Desemba 2012
wakati alipokutana na Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani ambao wamehitimisha
Mkutano wao wa Mwaka hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, uelewa makini kuhusu
binadamu unapata chimbuko lake katika Ufunuo sanjari na matumizi ya akili ya kawaida
inayobainisha haki na wajibu wa binadamu, kama alivyopembua kwa kina na mapana Papa
Yohane wa Ishirini na tatu.
Haki na wajibu ni chanda na pete kwani ni mambo
yanayotegemeana pamoja na kujikita katika msingi wa maadili ambayo yameandikwa katika
dhamiri ya mwanadamu na hivyo kupata mwelekeo sahihi wa mtu na jamii. Jamii nyingi
zinaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, lakini kwa
bahati mbaya, kwa upande mwingine, kuna ubinafsi na sera za uchumi tenge ambazo zinazombeza
mwanadamu.
Licha ya maendeleo ya mawasiliano ya jamii, lakini bado mwanadamu
wa leo anajikuta akiogelea katika upweke; kinyume kabisa na asili yake ambayo ni kiini
cha uhusiano kati yake na jirani zake pamoja na Mwenyezi Mungu. Mtu anajiona kuwa
ni rasilimali na sehemu ya mchakato wa shughuli za uzalishaji na ununuzi; mambo yanayomdhalilisha
utu na heshima yake.
Raha kupita kiasi na ubinafsi unaojionesha katika haki
za kujamiiana, uzazi, mtaji unaojikita kwenye faida kubwa ni mambo ambayo yanaathari
kubwa katika uchumi halisia. Mifumo hiii inamfanya mfanyakazi kuwa mtumwa wa kazi
na kazi yake kuwa na mafao kidogo katika Jamii, hali inayohatarisha misingi ya maisha
ya Familia. Binadamu katika asili yake, anaalikwa kuwaheshimu wengine, kulinda na
kutunza mazingira kwani anatambua dhamana aliyo nayo kwake binafsi na kuhusiana na
mazingira.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema kadiri ya Mafundisho
ya Kanisa, kazi ni msingi wa maisha ya binadamu, kama mtu binafsi na jamii; sanjari
na ushiriki wake katika kujenga familia, daima akitafuta mafao ya wengi pamoja na
kukuza amani. Fursa za kazi ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, hata
wakati wa kuchechemea kwa uchumi wa kimataifa.
Uinjilishaji Mpya wa Jamii unaweza
kumwibua mtu mpya mwenye kuthamini zaidi tamaduni na kutaka kuziendeleza. Ni mtu atakayesimama
kidete kupambana na ubinafsi, malimwengu na teknolojia kwa kukuza na kudumisha udugu,
hali ya kujitoa bila ya kujibakiza sanjari na mshikamano wa upendo; kwa kumwilisha
Amri ya Upendo kwa Mungu na Jirani. Hii ndiyo siri ya mabadiliko katika Jamii kitaifa
na Kimataifa.
Papa Yohane wa Ishirini na tatu aliichangamotisha Dunia, kujenga
Jumuiya ya Kimataifa inayojikita katika upendo kwa ajili ya mafao ya Familia ya binadamu,
kama anavyobainisha kwenye Waraka wake kuhusu Amani Duniani. Kanisa halina mamlaka
ya kutoa mwelekeo wa kisheria na kisiasa kuhusu mwelekeo mpya wa Jumuiya ya Kimataifa,
lakini linatoa mwono sahihi wa binadamu, maadili kwa ajili ya mafao ya wengi.
Hakuna
uongozi bora unaojikita mikononi mwa watu wachache tu, wanaowatawala wengine pamoja
na kuwanyonya maskini. Uongozi bora unajikita katika nguvu ya kimaadili, matumizi
sahihi ya akili pamoja na kuwashirikisha wengine mintarafu uwezo na haki husika.
Baba
Mtakatifu analishukuru Baraza la Kipapa la Haki na Amani pamoja na taasisi mbali mbali
ambazo zimejitahidi kueneza ujumbe wa Waraka wake wa kichungaji, Upendo katika Ukweli,
kama sehemu ya changamoto inayopania kuleta mabadiliko katika mfumo wa fedha kimataifa
kama watakavyofanya wakati wa Semina ya Kimataifa kuhusu Waraka wa Papa Yohane wa
Ishirini na tatu, Amani Duniani.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, amehitimisha hotuba yake kwa kuwaweka wajumbe wa Baraza la Kipapa la Haki
na Amani chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili aweze kuwaongoza katika
kutangaza na kushuhudia Mafundisho Jamii ya Kanisa.