2012-12-03 07:48:46

Tafakari kwa wanafunzi kutoka Roma wakati wa Masifu ya Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio


Wanafunzi kutoka taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu mjini Roma, Jumamosi tarehe Mosi Desemba 2012 waliungana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuanza hija ya kipindi cha Majilio kwa kusali pamoja Masifu ya Jioni, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio. Ifuatayo ni tafakari iliyofanywa kabla ya masifu ya jioni kama anavyotusimulia Sr. Gisela Upendo Msuya. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anabainisha kwamba, Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ni kipindi cha neema kinachotoa fursa kwa waamini kumrudia tena Mwenyezi Mungu kwa kuifahamu na kuimwilisha Imani yao kwa ujasiri mkubwa zaidi; sanjari na kuhakikisha kwamba, wanaendelea kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa, “Mwalimu wa Binadamu”; kwa njia ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Matendo ya Huruma.

Haya ni matendo yanayowawezesha waamini kukutana na hatimaye, kumfaham Kristo, Mungu kweli na Mtu kweli anayewaletea mabadiliko ya kweli katika maisha, kwa kujitambua kwamba, wao kweli ni watoto wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, kukutana na Kristo kunamwezesha mwamini kuboresha uhusiano wake wa kibinadamu na watu wengine, kwa kujielekeza zaidi katika mshikamano, udugu mintarafu upendo wa Mungu. Imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayogusa maisha ya mtu mzima, si tu katika akili na ufahamu wake; vionjo, moyo, utashi, mwili na mahusiano ya kibinadamu. Imani inaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mwamini kwa kumwonesha hatima ya maisha yake; ukweli wa wito wa binadamu katika historia; maana ya maisha pamoja na ile hamu ya kujisikia kuwa ni sehemu ya mahujaji ambao wako katika hija ya kuielekea Yerusalemu ya mbinguni.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, Katekesi zake katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani zinalenga kuimarisha furaha ya Imani kwa kuifahamu zaidi, kwani ni sehemu ya uhalisia wa maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Paulo wa Sita, katika Waraka wake wa kichungaji kuhusu Mitume Petro na Paulo “Petrum et Paulum Apostolos”, aligusia kwa namna ya pekee kuhusu kumong’onyoka kwa misingi ya Imani ndani ya Jamii. Kuna uelewa potofu wa kitaalimungu, kifalsafa na wakati mwingine kwa makusudi mazima, watu wanapenda kupotoshaMafundisho ya Kanisa na Kweli za Kiinjili. Kwa kufanya hivi wanadhani kwamba, wanakwenda hatua kwa hatua na ulimwengu mamboleo; wanafuata dira ya Viongozi wa Kanisa.

Mwelekeo kama huu anasema Papa Paulo wa Sita, unatikisa misingi ya Imani, fadhila za kimungu zinazoungamwa na kufundishwa na Mama Kanisa. Ndiyo maana viongozi wa Kanisa hawana budi kusimama kidete kuhakikisha kwamba, Mafundisho Tanzu ya Kanisa yanaeleweka mintarafu changamoto na mwelekeo uliotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, bila kupunguza uzito wake.

Kanisa lazima liendelee kuwa aminifu katika Mapokeo yake, kwa kutoa fursa kwa kila Mwanakanisa kumwelekea: Yesu Kristo Mwana wa Mungu, Mshenga na kielelezo cha utimilifu wa Ufunuo wa Mungu, Imani yake binafsi, kwa kusema kwamba, “Ninasadiki” kutoka katika undani wa: Akili, Utashi, Ubinadamu na utume wake kwa ajili ya wokovu wa wote. Ni wajibu wa Waamini kuwaheshimu Mitume Petro na Paulo, Miamba ya Imani na Mashahidi wa Kristo kwa kuendelea kuwaenzi katika hija ya Imani tendaji, daima wakichuchumilia umoja na mshikamano katika Imani.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, mabadiliko ndani ya Kanisa yanaletwa na ushuhuda unaojikita katika wongofu wa ndani, kwa kutangaza ukweli wa Injili, dhamana ambayo Wafuasi wa Kristo wamekabidhiwa kuiendeleza. Mwaka wa Imani, iwe ni fursa ya kutubu na kumwongokea Kristo, Mkombozi wa Ulimwengu.

Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ameonesha utimilifu wa upendo unaokoa kwa kuwaalika waamini kutubu kwa kuondolewa dhambi zao. Kwa njia ya Ubatizo, waamini wameifia dhambi na kuzikwa pamoja na Kristo; na kama alivyofufuka kutoka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba yake wa mbinguni, waamini pia wanaweza kuanza hija ya maisha mapya inayopata chimbuko lake katika Imani juu ya Kristo Mfufuka.

Baba Mtakatifu anasema, Upendo wa Kristo unawawajibisha, unawatuliza na kuwasukuma waamini kusonga mbele katika mchakato wa Uinjilishaji. Kama ilivyokuwa nyakati za mwanzo, hata leo hii, Kristo anawatuma wafuasi wake kwenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza Injili kwa Watu wa Mataifa yote. Hii ndiyo dhamana ya Uinjilishaji Mpya, inayopania kuwawezesha waamini kuwa na ari na mwamko mpya wanapoiungama Imani yao, kwa njia hii wanaimarika kwa kuamini, kama anavyosema Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa.

Kwa kuamini, Imani inakua na kuimarika; hakuna njia nyingine ya kuweza kuwa na uhakika wa maisha yako, anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika sehemu ya Waraka wake wa Kichungaji, Mlango wa Imani, kama si kujitoa bila ya kujibakiza mikononi wa Mungu ili kuonja upendo mkuu kwani unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.