2012-12-03 09:08:39

Majilio kiwe ni kipindi cha kukesha na kusali; kuendeleza Ufalme wa Upendo, Haki na Amani


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili iliyopita, tarehe 2 Desemba 2012, alielezea kuhusu Mwaka Mpya wa Liturujia ya Kanisa unaofunguliwa rasmi kwa Kipindi cha Majilio, ambacho kwa mwaka huu unatajirishwa na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni kipindi cha majuma manne yanayotangulia Sherehe ya Noeli.

Neno Majilio katika asili yake, lilionesha ujio wa Mfalme, lakini katika mazingira ya Kikristo lina maanisha ujio wa Mwenyezi Mungu duniani; Fumbo ambalo linagusa ulimwengu wote pamoja na historia yake: ni ujio wa kwanza unaojionesha katika Fumbo la Umwilisho na Ujio wa Pili ni pale atakapokuja kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu, wakati wa utimilifu wa nyakati. Ni matukio ambayo yanagusa: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo; matukio ambayo yameleta mabadiliko katika maisha ya mwanadamu na ulimwengu kama hitimisho la kazi ya uumbaji.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Habari Njema ya Wokovu haina budi kutangazwa hadi miisho ya dunia, ili ulimwengu uweze kuonja uwapo wake. Ujio wa Kristo kama ulivyotangazwa katika Injili, unamwalika kila mwamini na Kanisa kama mchumba wake, kushiriki kikamilifu ili kujiweka tayari kwa ujio wa Kristo.

Mwinjili Luka anawaonya wafuasi wa Kristo kujiangalia ili mioyo yao isije ikalemewa na ulafi, ulevi na masumbuko ya maisha haya; anawataka kukesha kila wakati huku wakiomba! Mkazo mkubwa ni watu kuwa na kiasi pamoja na kusali, daima wakijitahidi kukuza upendo kati yao na kwa ajili ya wengi, kama njia ya kutafuta utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anabainisha kuwa licha ya matukio mbali mbali yanayotisha duniani, watu kutojali pamoja na kumezwa mno na malimwengu, Wakristo wanaweza kupata wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wakitolea ushuhuda kwa njia ya utofauti wa maisha yao, kwani watapata utulivu na haki ya Mungu itaweza kutawala. Jumuiya ya waamini ni kielelezo cha upendo wa Mungu na haki yake inayotenda kazi katika historia, lakini bado haijafikia utimilifu wake; changamoto ya kuitumainia, kuiomba na kuitafuta kwa uvumilivua na ujasiri mkuu.

Bikira Maria aliweza kumwilisha ndani mwake moyo wa Majilio, kwa kuwa msikivu, daima akitamani kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake pamoja na utoaji wa huduma ya furaha kwa jirani zake. Mama huyu awe ni kiongozi, kwani Mwenyezi Mungu anayekuja, asiwakute wakiwa wamejifunga ndani mwao au wakitangatanga, bali kila mwamini akijitahidi kuendeleza Ufalme wa upendo, haki na amani.

Baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu alimkumbuka Mwenyeheri Devasahayam Pillai, mwamini mlei kutoka India, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 2 Desemba 2012 mjini Kottar. Aliishi kunako karne ya 18, akafariki dunia kama Mfiadini. Mama Kanisa anaungana na waamini nchini India kwa ajili ya kumshangilia Mwenyeheri mpya; ili aendelee kuimarisha imani ya waamini nchini India.

Tarehe 3 Desemba ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani. Baba Mtakatifu anasema kwamba, kila mtu hata katika ulemavu wake: kimaumbile au kisaikolojia ana thamani kubwa machoni pa Mwenyezi Mungu. Anawaalika waamini katika Jumuiya za Kikanisa, kuwa makini na daima wawe tayari kuwasaidia watu wenye ulemavu. Anawachangamotisha watunga sheria na viongozi wa serikali kuwalinda watu wenye ulemavu pamoja na kuwasaidia kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.