Changamkieni mikakati ya Uinjilishaji Mpya kama sehemu ya mwendelezo wa Jubilee ya
Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Enugu
Askofu mkuu Augustine Kasujja Balozi wa Vatican nchini Nigeria, katika maadhimisho
ya Jubilee ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki la Enugu, hivi karibuni, amewataka waamini
kujikita zaidi katika kupanga na kutekeleza mikakati inayotoa kipaumbele cha kwanza
kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya, kama changamoto endelevu katika maisha na utume wa
Kanisa.
Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Enugu yanakwenda
sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto ya kusoma
alama za nyakati kama walivyobainisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni
kipindi cha shukrani kwa Wamissionari na Waamini wa kwanza kwanza waliojitosa kimaso
maso kupokea Injili ya Kristo na kuendelea kuikumbatia kama dira katika maisha yao
kwa kipindi cha miaka hamsini iliyopita.
Jimbo la Enugu, Nigeria, limekuwa
na mafanikio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa ni mahali ambapo
kuna Seminari kuu ya Kanda, ambayo imekuwa ni kitalu cha majiundo ya Kipadre nchini
Nigeria na matunda yake yanaendelea kuonekana sehemu mbali mbali za dunia. Huduma
za Kanisa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ni kati ya mchango mkubwa
wa Jimbo Katoliki la Enugu kwa wananchi wa Nigeria.
Askofu mkuu Augustine
Kasujja anaialika Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Enugu, Nigeria, inapofungua ukurasa
mpya baada ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo hilo, kujikita zaidi na
zaidi katika Utangazaji wa Neno la Mungu sanjari na Uinjilishaji unaojikita katika
ushuhuda wa maisha amini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.