2012-12-03 07:59:43

Baba Mtakatifu anawaalika wanafunzi kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake hata katika mazingira yao!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi jioni, tarehe Mosi, Desemba, 2012, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amekianza kipindi cha Majilio kwa kusali pamoja na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vilivyoko mjini Roma, kama ishara pia ya kuanza kwa Mwaka wa Masomo 2012/2013. Kipindi cha Majilio ni mwaliko kwa waamini kugundua na hatimaye, kujitahidi kuishi kwa uaminifu Umungu wa Kristo atakayejifunua mjini Bethlehemu katika hali ya mtoto mchanga.

Historia nzima ya wokovu ni hija inayoonesha upendo, huruma na utashi wa Mungu: tangu kuumbwa kwa ulimwengu, hadi kukombolewa kwa Waisraeli kutoka utumwani Misri, kwa kupewa zawadi ya Amri za Mungu pale mlimani Sinai na baadaye kukombolewa kutoka utumwani Babeli. Mwenyezi Mungu daima ameonesha uvumilivu wa hali ya juu anasema Baba Mtakatifu, hata pale ambapo mwanadamu alimtenda dhambi; amemwonesha uhuru unaofumbata upendo wa dhati, kwa kuheshimu utu wake, akiwa tayari kumpokea anapomrudia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani.

Mwenyezi Mungu ameuangalia unyonge wa mwanadamu, akajinyenyekesha katika Fumbo la Umwilisho, kinyume kabisa cha matarajio ya binadamu; akaingia katika historia na maisha ya mwanadamu, akaandamana naye katika hija yake hapa duniani, kama kielelezo cha uaminifu wake kwa binadamu, daima akimtakia mema bila hata ya kujibakiza. Huyu ndiye Mungu ambaye ni upendo na kwa njia ya Yesu wa Nazareni, anaukumbatia ndani mwake ubinadamu wote na kuupatia mwelekeo mpya wa kuwa ni mwana mpendwa wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, ni furaha yake kuweza kuwashirikisha wanafunzi na majaalimu wao kutoka taasisi na vyuo vikuu vilivyoko hapa mjini Roma. Uwepo wao kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ni alama ya kurudia tena kuungama Imani yao kwa Kristo, sanjari na maandalizi ya utume na maisha yao ndani ya Kanisa na Jamii.Wasomi hawa walioko mjini Roma, kwa kushirikiana na viongozi wao wa maisha ya kiroho, wanayo nafasi kubwa ya kuweza kufanya hija ya sala, tafiti, upembuzi yakinifu mintarafu ushuhuda wa Injili, changamoto ya kuwa ni waaminifu kwa Mungu ambaye anapaswa kuwa ni mwamba wa maisha yao.

Kwa maadhimisho pamoja na kuishi na Kanisa zima, wataonja kwamba Yesu Kristo ni Mkombozi wa dunia na Bwana wa historia, bila yeye hakuna kinachowezekana. Wasomi wanaalikwa kujitahidi kuiishi kikamilifu Liturujia ya Kanisa, kwani ni shule itakayowawezesha kumwilisha Imani yao ya Kikristo, imani ambayo ni fadhila ya Kitaalimungu inayowakumbatia katika ukamilifu wao wote, ili waweze kuwa ni mawe hai katika ujenzi wa Kanisa na wadau wakuu wa azma ya Uinjilishaji. Kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwenyezi Mungu anajifanya kuwa karibu zaidi na waja wake na chakula chao cha njiani, kinachowaletea mageuzi ya ndani kwa njia ya upendo mkamilifu.

Baba Mtakatifu anawaambia wasomi hawa kwamba, hata kama vijana wengi wanaonekana kuwa mbali na Mwenyezi Mungu katika uhalisia wa maisha yao, lakini bado ndani mwao wana kiu ya uwepo wake, changamoto ya kumtolea ushuhuda katika maeneo ya taasisi na vyuo vikuu wanamosoma; wanapotafuta ukweli, kwani anawaangazia katika shughuli zote hizi.

Imani ni mlango ambao Mwenyezi Mungu anawafungulia waja wake ili waweze kukutana na Yesu na hatimaye, waweze pia kukutana na Muumba wao. Imani ya Kikristo inafumbatwa katika Mungu aliye hai, aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akakaa kwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kuamini ni kujishikamanisha na Kristo, ili kuonja tumaini lisilo na mwisho.

Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anawaalika wasomi wote walioko mjini Roma kushiriki kikamilifu, kwa kuendeleza majadiliano ya kina miongoni mwao, kwa kutambua kwamba, Kanisa daima limekuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu. Maadhimisho ya Wiki za Kitamaduni pamoja na Kongamano la Kimataifa kwa ajili ya Majaalim litakayofanyika mjini Roma, ni kielelezo cha dhamana hii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, makongamano kama haya yanaweza pia kufanyika sehemu mbali mbali za dunia.

Yesu anayewapenda na kuwathamini, anataka kuwatumia kuwa ni vyombo vyake vya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Masifu ya kwanza ya Kipindi cha Majilio ni mwanzo wa hija kuelekea mjini Bethlehemu, ili kuonja furaha ya Noeli, kwa kumpokea na kumweka Yesu kuwa ni kiini cha maisha yao, kama walivyofanya Maria na Yosefu. Jicho la Mungu liko wazi kwa kila mwanadamu, kwani ni mwaminifu katika upendo wake unaomkirimia mwamini amani ya kweli.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani itakayofanyika mjini Rio de Janeiro itakuwa ni fursa ya kuonesha uaminifu wao kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya ushuhuda unaojikita katika wongofu wa ndani, utu na maadili mema.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amewaweka wanafunzi wote wa Roma chini ya usimamizi na ulinzi wa Bikira Maria kikao cha hekima; masomo, maisha, lakini zaidi katika majiundo na ushuhuda katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani.









All the contents on this site are copyrighted ©.