Mikakati ya Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amerejea nyumbani kutoka Nairobi, Kenya ambapo
amehudhuria mkutano wa Viongozi wa Nchi za Jumuiya ya Africa Mashariki (EAC), mkutano
ambao umehitimisha vikao na sherehe mbalimbali za kufungua miradi ya pamoja ya nchi
hizi.
Katika mkutano wa tarehe 30 Novemba, 2012, Rais Mwai Kibaki wa Kenya
amemkabidhi rasmi Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uenyekiti wa Uongozi wa Jumuiya,
kikao ambacho kimehudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania
na Uganda.
Tarehe 27 Novemba, 2012 Rais Kikwete amehutubia Bunge la Jumuiya
ya Afrika Mashariki katika kikao chake cha tatu tangu kuzinduliwa rasmi mwaka huu.
Rais Kikwete amesema pamoja na changamoto zilizopo, Jumuiya inazidi kukua na kuimarika.
Tarehe
28 Novemba, 2012 Viongozi wa EAC wamezindua makao ya kudumu ya ofisi za EAC, sherehe
ambayo umehudhuriwa na viongozi wa nchi hizi ambapo mara baada ya uzinduzi wa jengo
hilo, viongozi wote wakaelekea Athi River na kufungua rasmi barabara ya Arusha - Namanga-
Athi River yenye urefu wa kilometa 240. Sherehe ambayo pia umehudhuriwa na Rais Piere
Nkurunziza wa Burundi ambapo Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda
wamewakilishwa na Mawaziri wao Wakuu. Katika ufunguzi huo, Rais Kikwete amesema Jumuiya
hii ni muhimu na yenye manufaa makubwa kwa nchi hizi.
Tarehe 29 Novemba, 2012
viongozi wamekutana katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta na kuzungumzia
miradi mbalimbali ya miundombinu ikiwemo, barabara, reli na bandari , miradi ambayo
kwa pamoja itahudumia na kunufaisha wananchi wa nchi hizi.