2012-12-01 07:38:04

MAJILIO: Ni kipindi cha kukesha kwa Sala, Maisha ya Kisakramenti, Tafakari ya kina na Matendo ya huruma!


Moja ya hadithi nzuri za Esopo, tulizokuwa tunasoma shule ya msingi ilihusu kijana mchungaji na kondoo. Kijana huyo alikuwa kila mara anaenda peke yake kuchunga kondoo wa baba yake. Huko malishoni hakukuwa na mtu wa kucheza naye. Kutokana na upweke, alijisikia kuchoka au wasemavyo waswahili, alijisikia “kuboreka.” Baada ya kuwaza na kuwazua, akagundua jinsi ya kujichangamsha na kujitoa uvivu kwa upweke huo.

Akagundua mbinu ya kuwaita watu kufika machungani. Siku moja, akapanda kwenye mti na kugumia: “Chui, chui, chui, njooni, njooni jamani mniokoe.” Wakaja mbio, wanaume wengi wenye nguvu wamebeba mikuki na marungu ili kumnusuru yule kijana. Walipofika wakamwuliza: “Chui yuko wapi?” Kijana akawajibu kwa utulivu huku akijizuia kucheka: “Nadhani chui amesikia vishindo vyenu, ametoroka”. Wale watu wakarudi huku wakisikitika wamepoteza muda wao.

Baada tu ya wale watu kuondoka, kijana akaanguka kicheko na kujisifia kwamba mchezo wake umefanikiwa. “Mlamba asali halambi mara moja tu.” Siku nyingine, kijana akacheza tena mchezo uleule. Akapanda juu ya mti na kuita: “Chui, chui, chui, njooni, njooni jamani mniokoe.” Wanaume wakaja na silaha zao bila kumwona chui, na kijana akatoa tena hoja ileile kuwa chui amekimbia. Wale watu wakatikisa tu vichwa vyao, wakagundua kuwa kijana alikuwa anacheza.

Mmoja wa wanaume wale akajisemea peke yake: “Sina muda wa kupoteza kucheza. Sitafika tena huku porini.” Kwa hiyo mara hii mchezo wa kijana haukupita vizuri. “Mzaha mzaha hutumbua usaha.” Ikatokea siku nyingine majira ya jioni, kijana akamwona chui akinyemelea kondoo ili kuua. Kijana akaogopa, akakwea mtini na kuanza kulia kwa sauti kuomba msaada: “Chui, chui, chui, njooni, njooni jamani mniokoe.”

Wanakijiji waliposikia sauti ya kijana, wakatulia tu! Wakijua kwamba ni kawaida yake ya kucheza. Yule kijana akaendelea kulia kwa nguvu na kusisitiza: “Jamani, jamani si utani chui anaua kondoo, Njooni njooni, mniokoe.” Wanaume wote kijijini wakabana tu kimya hakuna aliyeshtuka kwenda kumwokoa. Chui akamkamata kondoo mmoja akamwua na kumvutia porini zaidi. Kijana aliporudi nyumbani na kondoo waliobaki, aligombezwa sana na baba yake na kuambiwa: “Ukishatambulika kuwa ni mwongo hakuna atakayekuamini hata pale utakapokuwa unasema ukweli.”

Hadithi hii, inatuhusu sisi wakristu hasa kipindi hiki cha Majilio tunachotegemea kukiishi kwa wiki nne tu, na baadaye inafuata sikukuu ya Noeli au Christmas (kuzaliwa kwa Kristo). Baada ya kumaliza kuitafakari Injili ya leo, fundisho la hadithi hii litaeleweka lenyewe bila maelezo zaidi.

Leo ni dominika ya kwanza ya Majilio ndiyo ni mwanzo wa mwaka wa liturujia. Leo tunaacha mwaka wa Marko (B) na kuingia mwaka wa Luka (C). Katika Injili ya leo Luka anayatafsiri mafundisho ya Yesu juu ya siku ya mwisho au siku ya kiyama ili kuyafanya yaeleweke na kuwa na maana kwa wasomaji wa wakati wake, waweze kuiishi kwa dhati imani yao.

Ukweli ni kwamba fasuli ya leo toka Injili ya Luka, ilishasomwa wiki mbili zilizopita toka injili ya Marko. Luka aliandika Injili yake miaka mingi baada ya kuandikwa Injili ya Marko. Hivi Luka aliijua Injili ya Marko na akayachukua mawazo mengi toka Marko na kuyaingiza katika Injili yake, ila si kwa mtindo wa "kukopi na kupesti". Luka alifanya marekebisho kadhaa na ya muhimu ili yawafae wasomaji wake kwa wakati na katika mazingira ya hali halisi ya maisha waliyokuwa wanayaishi.

Mfano mdogo wa nukuu na marekebisho hayo ya Luka, tunauona katika muujiza ule wa kuponywa mtu aliyepooza: Marko anatueleza kwamba waliomchukua mgonjwa walibomoa dari au paa ya nyumba. (Mk. 2:4), kumbe Luka katika Injili yake anasema watu wale walitoa vigae vya dari au vya paa ile ya nyumba (Lk. 5:19). Kwa hiyo, Marko alikuwa na wazo la nyumba ya Kipalestina ambayo kwa kawaida ilikandikwa udongo. Kumbe Luka, ana wazo la nyumba ya kirumi iliyoezekwa vigae.

Kadhalika, tunaposoma leo fasuli toka Injili ya Luka kuhusu mafundisho ya Yesu juu ya siku ya kiyama. Tuangalie vizuri sana jinsi Luka anavyokielezea kituko hicho kitakavyokuwa ukizingatia anataka kutilia mkazo wazo kuu gani juu ya siku ya kiyama.

Ukiipambanisha Injili ya Marko ilivyosomwa dominika ya 33 na Injili ya leo, unamwona Luka anaacha vituko vingi vya kutisha alivyoviandika Marko. Marko anaorodhesha patashika itakayotokea angani siku ya kiyama: “Siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika.” (Mk. 12:24-32).

Kumbe Luka anaacha kuandika matisho hayo badala yake anasema tu kifupi: “Siku ile kutakuwa ishara katika jua; na mwezi na nyota” (Luka 21:25). Aidha, anaacha kabisa wazo analoliongeza Marko anaposema: “Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.” (Mk. 13:27). Badala yake Luka anasema: “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi na masumbufu ya maisha haya;” (Luka 21:34)

Kwa nini basi Luka anaacha kuandika vituko hivyo vya kutisha ambavyo ni rahisi kuviona na kuvifafanua kama anavyofanya Marko? Ninaona Luka anafanya hivyo kwa hoja moja tu muhimu, kwamba kwa wakati wake mambo au hali halisi ya maisha ilikuwa imebadilika, hivi akawa anaona mambo kwa mtazamo mzuri zaidi.

Ikumbukwe kwamba Marko aliandika Injili yake mwaka 70 BK, yaani kabla ya kuangua kwa hekalu la Yerusalemu. Nyakati za Marko, Wakristu-wayahudi walikuwa na uhakika kwamba kuanguka kwa Yerusalemu na kubomolewa kwa Hekalu la Yerusalemu kungeenda sambamba na mwisho wa dunia. Kinyume chake, kuanguka kwa Yerusalemu kukafika na kukapita ulimwengu ukabaki ngangali bila kubomoka.

Kwa hiyo, kuanguka kwa Yerusalemu na kubomolewa Hekalu kuligusa na kuyumbisha sana imani ya wakristu wa awali. Mapato yake watu wengi wakaacha kabisa kuwa na imani ya ujio wa pili wa Kristu. Wakaanza kutulia, na kujichana kwa kula na kunywa na kulegea kabisa kimaadili. Changamoto kwetu sisi leo, kwamba mazingira ya mtindo huo ya kuunganisha vituko vinavyotisha na mwisho wa dunia ni vya kutoka zamani na unaweza kuona vikitokea hadi leo. Vituko hivyo vinateteresha sana imani hata kupotosha maadili. Kwa hiyo sasa Luka anapoandika mwaka wa 80 BK, anayo nafasi nzuri ya kuona ukweli wa mambo kuliko alivyokuwa ameona Marko.

Ili kueleza ukweli zaidi kadiri ya hali halisi ya wakati wake, na kuwaepusha waumini kuangalia juu angani, Mwinjili Luka akaongeza sehemu ya pili, akiwaonya wakristu na kusema: “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi na masumbufu ya maisha haya;” (Luka 21:34) Neno hili ulafi linamaanisha hali ya kukinai unayoipata mtu baada ya kula na kunywa mno.

Ndugu zangu, Majilio ni kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa Bwana kwanza ile siku ya mwisho kabisa atakapofika, na ujio ule wa siku ya Noeli ambayo ni ukumbusho wa kuzaliwa kwake miaka elfu mbili iliyopita. Katika kipindi hiki tunafanya vyema kumwimbia Kristo Masiha nyimbo za kumwita: “Njoo Masiha, Njoo Masiha, Njoo Masiha utukomboe.” Masiha huyo anapofika Noeli anategemea tumweleze atunusuru toka hatari gani, au tumweleze kitu tulichomwitia au walao tumwoneshe imani yetu tunavyoiishi kila siku. Kumbe, siku hiyo sisi tunafanya yaleyale ya kijana mchungaji, tunaangua kicheko, tunajichana na kulemewa na ulafi na ulevi.

Mwinjili Luka leo, anatukumbusha namna nyingine ya ujio wa Kristo ambao tunaelekea kuusahau, na kujiingiza kwenye kuangua kicheko na kujichana wenyewe tu, nao ni ule ujio wa Kristu wa kila siku katika matukio ya kawaida ya kila siku, na ujio wa Kristo katika wenzetu. Ujio huu ndio unaodai kuwa na imani sana kuupambanua na kuuishi. Msisitizo wa Luka ni huu kwamba inabidi tukeshe au tujiangalie, tutambue na kumpokea Bwana anayetujia kila siku katika watu tunaokutana nao.

Tumtambue Bwana anayetujia mahali na katika matukio tusiyoyategemea, hususani matukio yale tunayofikiri kuwa tunaonewa. Hii ndiyo imani ya kweli ya kusoma ishara za nyakati na siyo kuangalia juu kwenye vituko vya kutisha, bali kuangalia chini kwenye maisha ya kila siku.

Endapo sisi tunajiandaa kwa ujio wa Bwana kwa kutazama juu, Mwinjili Luka leo anatualika kuangali kila pahala, kungalia katika historia ya maisha yetu ya kila siku, na kumtambua Bwana anayetujia kwa njia ambazo hatuzitambui kabisa. Baada ya kutambua ishara hizo tuishi kwa dhati imani yetu kwa matendo ya dhati na siyo kwa unafiki. “Ukijulikana kuwa ni mwongo, hakuna atakayekuamini hata pale utakapokuwa unasema ukweli.”

Mama Maria, Mama wa imani atuombee na kutufundisha kuwa wa kweli katika imani yetu.

Tafakari hii imetayarishwa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.