2012-12-01 08:00:14

Elimu ipanie kumkomboa mwanadamu kwani hii ni sehemu ya maisha!


Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Padre Reginald Mrosso, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, wakati wa kuwaaga wahitimu wa masomo ya ufundi stadi, kutoka Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspar, kilichoko, Manyoni, Singida, Tanzania, tarehe 1 Desemba 2012.

Ndugu wapendwa, leo tumekusanyika hapa ili kuwaaga au ningesema kwa lugha inayofaa zaidi kuwapongeza wapendwa wetu hawa ambao wanahitimu awamu moja katika harakati zao za kujikomboa kielimu.

Hongereni sana. ni vizuri kwa ye yote yule anayefanya jambo jema kupewa pongezi na kupewa msukumo wa kuendelea mbele. Nasi leo hii tupo hapa lakini nia kuu ikiwa ni kuwapa msukumo zaidi wa kuendelea mbele. Hatua moja inaanzisha nyingine. Shukrani za pekee zimwendee mwenyezi mungu kwa mema aliyotujalia na kuweza kufika siku hii ya leo.

Shukrani kwa uongozi w a Shule kwa usimamizi mzuri uliopelekea haya yote kufanyika. Shukrani kwa wazazi, walezi, ndugu, jamaa, marafiki na wafadhili wetu wote ambao wametuwezesha kufanikisha mambo mbalimbali yanayotuwezesha kuwa hapa siku hii ya leo na yote yanayoendelea hapa. Shukrani kwa Uongozi w a shule na wafanyakazi wote kwa usimamizi mzuri uliopelekea haya yote kufanyika. ukiona vyaelea basi ujue vimeundwa. na jambo lo lote zuri humaanisha kuwa jasho limetoka Na kwa namna ya pekee tunawapongeza ninyi wahitimu kwa kiwango hiki cha elimu mlichofikia leo.

Haja ya elimu na kusoma ni hitaji mojawapo kabisa la mwanadamu. Wajibu wa mzazi ni kumfunza mwanae na mwana pia anafanya bidii yo yote ile ili kujifunza – angalia mtoto mdogo anavyojifunza kusema, kutamka, kufanya kitu fulani n,k. Ikitokea kuwa mtoto anachelewa kusema, kutamka maneno ya msingi, kujifunza au kufanya kitu fulani kadiri ya umri wake na makuzi yake basi wazazi au walezi wake hupatwa na wasiwasi na hata kutafuta namna mbadala ya kuweza kufanya au kumwezesha aweze kufanya au kujua kulingana na umri wake.

Mhu. 7:25 – basi, nikageuzia mawazo yangu kwenye elimu, niliitafuta na kuifuata hekima na akili, basi nikafahamu kwamba ubaya ni ujinga, na upumbavu ni wazimu. Mwenye ujuzi wa elimu anapata ukombozi toka mambo mbalimbali. Anaweza kushinda ujinga, upumbavu, dhambi na mambo kama hayo ambayo ni kinyume kabisa na utu wa mwanadamu.

Jukumu kubwa la mwalimu ni kufunza au kutoa elimu. Yule anayefika hapa – chuoni yaani mwanafunzi, anafika kwa lengo hilo tu yaani kufunzwa. Kinyume chake ni kwenda kinyume na malengo yako na uwepo wa nafasi hii. Sisi tunaamini kuwa ninyi mnaohitimu leo, mmetumia vizuri nafasi hii mliyoipata ambayo wapo vijana wenzenu wengi na ambao mnawafahamu waliotamani kupata nafasi kama hii lakini kwa sababu moja au nyingine na kubwa ikiwa umaskini wa wazazi na/au walezi wameikosa.

Pengine ni vizuri ninyi mnaohitimu leo hii kujiuliza – mmejifunza nini? kuna tofauti yo yote katika maisha yako kwa kipindi ulichokaa hapa – kabla na baada ya kupata nafasi hii? upo msemo kuwa waweza kukaa kwenye maji lakini usitakate. Mimi siamini hali hiyo kuwa kati yenu hapa. Muda miliokaa hapa wengine miaka miwili, wengine mitatu haiwezi ikawa tupu.

Ndio maana tuko hapa ili kuwapongeza na tunaamini kuwa mmeongeza idadi ya wasomi katika katika jamii yetu na taifa zima. Tunawadai kwa hilo. Bila shaka miaka hii ya elimu mmeitumia vizuri. Mmetumia muda na fedha za wazazi, walezi au wafadhili. Mna deni. Kuna waliojinyima kwa namna moja au nyingine ili ninyi msome. Hamna budi kuwashukuru.

Na namna moja ya kuonesha shukrani kwa jamii ni katika matumizi mazuri na kuishi vizuri katika jamii kile ambacho mmesoma. Msomi mmoja John Dewey anasema "Education is not preparation for future life but it is life itself". Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarahe Nyerere alitufundisha wakati fulani “jifunze kusoma, wakati ni huu”. Maana yake ni kwamba wakati wo wote ni wakati wa kujifunza na kutafuta elimu.

Wapendwa vijana, tumieni vizuri elimu hii mliyoipata. mara nyingi jamii inasikitika sana pale msomi anapoenda kinyume na ufahamu wake. Mwenye elimu au ufahamu au ujuzi wa jambo fulani anadaiwa kuutumia vizuri ujuzi huo. Kinyume chake ni kudharau kile ambacho umekipata. Elimu hutoa mwangaza kujua jema na baya, kuharakisha au kutatua shida kwa haraka, kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali n,k.

Hilo ndilo lengo la elimu na uwezo wake. Inasikitisha pale ambapo elimu hutumika kinyume cha lengo tarajiwa. Angalia wengine wanavyotumia vibaya kompyuta – kuiba, kuangalia picha za ajabu ajabu, fundi anapofunga spea feki, vifaa katika gari, vifaa duni vya umeme na hatima yake ni kuunguza nyumba na maisha ya watu ; vitu vya thamani kubwa. N.k. hilo ndilo lengo la elimu?

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anataja rasmi adui mmojawapo katika Taifa letu na maisha ya mwanadamu kuwa ni ujinga. Ujinga ni kukosa elimu. Elimu inakujengea uwezo wa kufikiri, inakupatia utatuzi wa jambo na namna ya kulitatua, kujiamini kwa kile unachofanya. Elimu inakupa nafasi ya kuchambua na kuchimba mambo na kuweza kueleza jambo kwa ufasaha. Elimu ni ufunguo wa maisha. elimu ni mwanga, elimu ni uhai.

Baada ya kuwafunza wanafunzi wake – Yesu Kristo katika – Mt. 28:19-20 – anawatuma Wanafunzi wake - ‘Basi, nendeni mkayafanye mataifa yote kuwa wafuasi mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Mkawafundishe kushika yote niliyowaagiza. Na tazama nipo nanyi siku zote mpaka mwisho wa dahari’.

Mt. Gaspar del Bufalo, ambaye shule hii ina heshima ya jina lake, aliishi utume huu. Tunasoma habari ya maisha yake kuwa katika ujana wake alionesha mwelekeo wa kufundisha kama katekisimu kwa wasioijua na kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa mahospitalini.

Watanzania wengi wanapenda njia ya mkato. Hakuna njia ya mkato katika maisha. Watu wengi wanapenda maisha bora bila elimu bora, bila kutoka jasho, bila uaminifu, bila elimu bora na utendaji bora. Wengi wetu tunataka kupata harakaharaka bila kupitia njia halali. Hakuna hilo. Unataka kuishi vizuri, soma vizuri. Nilisikia kipindi cha Jahazi siku moja wakishauri vijana “mitihani imekwisha sasa msiingie vijiweni. Saidieni wazazi kusukuma gurudumu la maisha".

Je, ni nani atatusaidia kutatua ugumu wa maisha? Tunaongea kuhusu tatizo la mazalia ya mbu katika mazingira yetu, Je, tunataka Wageni toka nje waje wazibue mitaro iliyoziba? Wafyeke majani katika maeneo ya nyumba zetu na mazalio ya mbu? Au Mwenyekiti wa Serikali ya mitaa aje afukie kifusi kilicho mbele ya nyumba yako? kumbuka kuwa mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe.

Mawaidha machache:
Ninyi Wa veta, naamini kuwa mmefundishwa tu si ufundi bali pia taratibu na maadili ya kazi na nidhamu ya kazi, namna ya kuandika barua ya kuomba kazi, viwango vya mishahara kadiri ya elimu uliyonayo, adhabu za utoro kazini n.k. Kumbukeni ule wimbo maarufu "nidhamu ya kazi ni msingi wa mafanikio mema kazini". Usiriridhike na ulichopata. kumbuka kuwa elimu haina mwisho.

Inasikitisha kukutana na fundi, tuseme fundi mekanika amevaa tai muda wa kazi. kuna muda wa kazi ambao unakubalika kijamii n.k. Ni aibu na kielelezo kikubwa cha umaskini. mawazo mengi ya watanzania ni kupata ajira, ya harakaharaka na inayolipa. Kumbuka kuwa ajira ya kwanza ni elimu yako, ni wewe mwenyewe, ni kichwa chako. hiyo ndiyo ajira ya kwanza. ukisahau hili umekwisha.

Kumbuka mojawapo ya falsafa za maisha na kazi, kazi yako ni jina lako. kumbukeni kuwa elimu haina mwisho. Fundi mahiri katika mazingira yake huwa hafahamiki au hajulikani kwa jina lake bali hujulikana kwa kazi yake. Watu wakihitaji huduma yake utasikia - nitafutieni yule fundi maji, mekanika na hata watu wakimuagiza hutaja eneo au mahali pake pa kazi. kweli si kweli?

Mshauri mmoja wa masuala ya maisha anasema – unafanyaje ikiwa mteja wako hanunui bidhaa yako? Anasema mpe nafasi yeye kwanza, halafu wewe weka bidhaa yako. Ukimwonesha wewe kile unachopenda na ikiwa siyo hiyo basi umempoteza. Akipata bidhaa anayotaka basi umempata na kesho atarudi tena kwako. Hapo umempata mteja wako.

Tujifunze pia kwa wengine jinsi wanavyofanya kazi na tuna mifano mizuri tu katika mazingira yetu. Tusibaki tu kuwasifia wengine “ Ona Wajapani bwana, Waitaliano, Wachina sijui nani sijui nini. kwa nini hii isiwe changamoto kwetu? Kama kweli kile wanachofanya ni kizuri kwanini basi nasi tusifanye kazi kama wao. tutaendelea kuwasifia wengine mpaka lini?

Tuondoe dhana mbovu kati yetu kwamba aliyendelea basi ameiba. kumbukeni fundisho kuwa asiyefanya kazi na asile. Na pia bila kusahau ili uweze kuwa na uhalali katika utendaji wako na kuwa na haki ya kupata chakula ni lazima ufanye kazi muda usiopungua saa nane (8) kila siku. huu ni utafiti wa kitaalamu na kisayansi kabisa. Hii ina maana kuwa kama mtu mzima na mwenye lazima ya kufanya kazi, asipofanya hivyo basi ana kosa. unastahili hukumu. Hivi kipimo cha msomi wa tanzania kipo katika nini? Katika kufaulu vizuri tu darasani au katika matumizi ya elimu iliyopatikana?

Unapokuta fundi seremala anayechonga milango vizuri lakini ana sifa mbaya ya wizi, ulaghai kwa wateja, atapata kazi kwa urahisi? Ataaminika na jamii? Inasikitisha sana pale ambapo fundi mzuri na mahiri anakuwa na maisha magumu kusiko mfano. Sababu ni mwizi, mlaghhai, mvivu, mbabaishaji n.k. Mwanafunzi ambaye darasani anapata alama 100 kwenye masomo yake lakini hawezi kuhusianisha elimu na uhalisia wa maisha maana yake nini?

Msomi anayetupa taka hovyo au kuchafua mazingira hovyo bila kujali - maana yake nini? Elimu inakupa nafasi ya kuwa na mpangilio, kinyume chake elimu inatumika kuchafua mazingira. Ni upi uhusiano wa elimu na uhalisia wa maisha?

Wanafalsafa wa zamani walisoma, kutafiti na kufundisha wengine ile elimu iliyohitajika ili kuujua ulimwengu. Ili kuweza kuishi vizuri. mwenye ufahamu ana nafasi ya kutawala. tumia elimu yako kujikomboa. Kutawala maisha na kujenga maisha bora. hakuna maisha bora bila kutoka jasho. Ikiwa hivyo, yaani kupata bila jasho basi utaingia kwenye kundi la wezi, mafisadi na watu kama hao.

Fanya kazi kama mtumwa ili uishi kama tajiri. Mchumia juani hulia kivulini. Misemo hii isizoeleke tu midomoni bali itutafakarishe sana. Tujifunze pia kwa waliotutangulia na wanaofanya kazi vizuri na inavyopaswa. Niwatakie heri na baraka tele.
Asanteni sana.
Padre Reginald Mrosso, C.PP.S, Mkuu wa Shirika, C.PP.S, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.