2012-11-30 15:29:21

Kwa nini Ufukara - Kardinali Turkson ajibu ....


Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Haki na amani , Kardinali Peter Turkson, ametajwa kuwa katika ziara ya kuzungukia mataifa duniani , kusikiliza utendaji wa jamii katika kupambana na umaskini, njaa na maradhi.
Nia ya ziara yake ni kushirikishana mawazo na uzoefu, na pia kuufikisha msaada wa Kanisa kupitia uzingatia wa mafundisho ya Kanisa ya kijamii yanayolenga kufanikisha amani na haki za binadamu, dhidi ya ukosefu wa haki na unyanyasaji.
Alhamis, akihojiwa na Redio Vatican juu ya Kampeini ya Vyombo vya mawasiliano iliyozinduliwa Alhamis 29 Novemba 2012, yenye Mada: Kwa Nini Umaskini ? Kardinali Turkson amekiri kwamba, lengo la maendeleo ya Millenia la kupunguza kwa nusu umaskini ifikapo 2015, ni wazi halitatimizwa. Dalili zinaonyesha bado linadorora nyuma, kwani bado kuna maskini wengi wanaoishi chini ya dola moja kwa siku kwa mtazamo huo. .
Aidha Kardinali alizungumzia maana ya umaskini akisema, mara baada ya kutangazwa lengo la kupunguza umaskini ifikapo mwaka 2015, kumekuwa na tafasiri nyingi juu ya hali hii, ikiwemo kujaribu kufafanua maana halisi ya neno maskini. Baadhi wametoa hoja kwamba, badala ya kulenga katika maana ya kuishi chini ya dola moja kwa siku, badala yake tathimini zizingatie, mitazamo ya mafanikio katika viwango vya elimu, huduma za afya na ustawi wa jamii katika maana ya maisha bora.
Na kwamba , maana msingi ya utu wa binadamu imefumbatwa katika aina mbalimbali za haki za binadamu , haki ya maisha bora, huduma ya afya ,ajira, ikiwemo pia haki ya kupata nishati na maji safi, vyote vikilenga katika maisha bora.
Na akitaja mchango wa Kanisa, katika juhudi za kufuta umaskini duniani , alisisitiza mshakamano wa kijamii akisema , “hakuna anayeweza kukanusha maumbile ya binadamu ya kutegemeana mmoja kwa mwingine “. Na ndivyo mafundisho ya Kanisa ya Kijamii yanavyosisitiza mshikamano wa kijamii katika juhudi zote za kuboresha maisha ya mtu iwe kihali au kiroho.
Aliyataja mafundisho ya Kijamii ya Kanisa, kuwa ni asili ya imani Mkristu, anayotakiwa kuishuhudia, yaani upendo wa Kristu, unaomjali kila binadamu, kuwa ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ambaye ndiye upendo. . Na hivyo Kanisa ni wajibu wake, kujihusisha katika mfumo wa kijamii kwa ajili ya ufanikishaji maisha tulivu, iwe kisiasa au shughuli za kiuchumi. Kazi kubwa waliyo nayo Wakristu, ni kufanya mafundisho ya Kanisa ya Kijamii yajulikane zaidi.








All the contents on this site are copyrighted ©.