2012-11-30 07:42:57

Kanuni Mpya ya Misa kwa Lugha ya Kiswahili Yaanza Kutumika


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaanza kutumia Kanuni Mpya ya Misa, iliyofanyiwa marekebisho katika lugha mbali mbali na kuanza kutumiwa na Kanisa kwa mara ya kwanza, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio mwaka Be wa Kanisa, yaani kati ya Mwaka 2011-2012. RealAudioMP3

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara ambaye pia ni Mwenyekiti, Idara ya Liturujia, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, Kanuni Mpya ya Misa kwa Lugha ya Kiswahili inaanza kutumika rasmi hapo tarehe 2 Desemba 2012, yaani Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2012-2013. Mabadiliko haya msingi yanapania kutoa tafsiri makini na aminifu ya Kanuni ya Misa, kwa kuzingatia machimbuko yake kutoka katika Lugha ya Kilatini.

Nchini Tanzania, tafsiri ya Kanuni Mpya ya Misa, imechelewa kutokana na uhaba wa Wataalam wa Liturujia na hivyo kuifanya tafsiri hii kuchelewa kuanza kutumika rasmi kama ilivyopangwa hapo awali. Kwa sasa tafsiri imekamilika baada ya kufanyiwa marekebisho na mazoezi katika Majimbo mbali mbali nchini Tanzania.

Askofu Libena anapenda kuchukua fursa hii, kuwahimiza Maaskofu wenzake, Mapadre na Taasisi mbali mbali nchini Tanzania kuanza kutumia Kanuni Mpya ya Misa kuanzia sasa. Kazi ya kutfasiri Misale ya Altare inaendelea kwa kasi na mara itakapokamilika, Kanuni Mpya ya Misa itaweza kuingizwa na hivyo kuunda Kitabu Kimoja tu. Kwa sasa anasema, Askofu Libena, Mapadre wataendelea kutumia Vitabu viwili, yaani Kanuni Mpya ya Misa na Misale ya Altare ya zamani, hadi pale zoezi zima litakapokuwa limekamilika.








All the contents on this site are copyrighted ©.