2012-11-29 14:08:07

Ujumbe kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wakati wa kipindi cha Noel


Askofu Msaidizi Lorenzo Leuzzi, wa Jimbo la Roma, Ofisi ya Kazi za Kichungaji , kwa ajili ya Vyuo Vikuu, ametoa barua yake ya kichungaji kwa wanafunzi wa Vyuo VIkuu jimboni mwake.

Barua hiyo ya kichungaji iliyowaita wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuwa kizazi kipya cha Wapendwa wa Yesu, imehimiza wanafunzi hao, wanaporudi nyumbani kwa ajili ya sherehe za Noel, wajawe na nyuso za furaha na tumaini, katika ukimya wa kusikiliza, kama ilivyo kuwa kwa Mtakatifu Francis na Clare!

Na kwamba hakuna jambo kubwa wanalotakiwa kutenda, isipokuwa kuwa na utulivu wa kusikiliza na kufurahia kurejea tena katika nyumba ya Baba, mwenye kuona mbali na mwenye kuonyesha mwelekeo wetu, kama Francis alivyosema, huu ni muujiza pekee wa uwepo wetu.

Askofu Lorenzo ameendelea kuasa kwamba Roma, kama ilivyo kawaida ya miji mikubwa, kuna makelele mengi ya kila aina na harakati nyingi zinazomfanya mtu ajiulize kama anaweza kuliishi upya fumbo la Noel, katika hali ya ukimya na utulivu. kutokana na hali hizo za harakati za kimji, ni muhimu kujipanga sawasawa katika kuutumia wakati. Kama Kant alivyosema, , "Wakati ni zawadi! Mimi si wakati , lakini ninapaswa kuutumia wakati, ili niweze kuuona uwepo wangu, na ili kufurahia maisha yangu. Nani anaweza kujaza wakati wangu"?

"Kwanza ni kujiepusha na purukushani na machafuko. Kwa kuwa anayeishi kwa kujiheshimu mwenyewe na wengine pia , huweza kuutawala wakati. Ni suala la kuona kwamba, kuna wakati kwa kila kitu: wakati kwa ajili ya utafiti, kwa ajili ya sala na ibada, kwa ajili ya familia na marafiki, kwa ajili ya kubadilishana mawazo na wengine na pia wakati kwa ajili ya kulala!
Askofu Lorenzo ameutazama kwa kina wakati wa kulala usiku, ambayo ni kawaida ya maumbile, akiutaja kuwa ni wakati tuliyopewa wa kupumzika! Kila mtu, kila siku baada ya kazi zake, anahitaji kupumzika! Na baadaye kuifungua siku mpya na furaha mpya , katika kuunza tena mzunguko wa siku na maisha.
Ujumbe wa Askofu umeelekeza mawazo pia katika usiku wa Noel, ambamo katika ukimya wa usiku, nuru iliangaza, kwa ajili ya ujio wa Mungu. Usiku ambao katika majengo mengi ya monestri za waamini, wake kwa waume, hubaki macho na Bwana, wakifanya hivyo pia kwa niaba yetu sisi , na kutukumbusha juu ya ujio wa Bwana , wakituwezesha kulala shwari. Wanastahili shukrani zetu!
Na pia amerejea tukio jingine la Injili , linaloturejesha katika mtazamo mwingine wa mapumziko ya usiku. Wakati Yuda aliamua kumsaliti Yesu, aliondoka chumbani kama mwinjilisti Yohane alivyoandika , ilikuwa usiku! (Yohana 13:30).

Askofu amekamilisha ujumbe wake, kwa kuwahimiza wapendwa wanafunzi wa vvyuo Vikuu, zaidi ya yote, katika kipindi hiki cha maandalizi ya ujio wa Bwana, kutembea pamoja na Papa Benedikto XV1, wakati wa Ibada, bila ya kuwa na woga wa giza la usiku, kwa kuwa wakati umetimia wa Neno kufanywa Mwili katika tumbo la Maria. Na katika hali ya ukimya wa usiku Mwanga unag'ara na kutuamsha , kama wazazi waamkavyo alfajiri na kuamsha watoto wao waliolala vitandani.







All the contents on this site are copyrighted ©.