2012-11-28 08:59:50

WAWATA ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; changamoto ya waamini walei kuyatakatifuza malimwengu!


Ifuatayo ni risala ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, wakati wa maadhimisho ya maonesho ya Miaka 40 tangu ilipoanzishwa. Kwa ufupi, risala hii inagusia kwa ufupi: historia ya WAWATA katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, taswira, malengo pamoja na utekelezaji wa utume wao ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Mwadhama Policarp Kardinali Pengo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dsm na Rais wa SECAM,
Mhashamu Askofu Mkuu Francisco M. Padilla Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania,
Mhashamu Askofu Desderius Rwoma –Mwenyekiti wa Idara ya utume wa Walei katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,
Waheshimiwa Mapadri na Watawa wa Kike na Wakiume,
Waheshimiwa Wageni wetu kutoka nchi za nje
Waheshimiwa Viongozi wote wa Halmashauri ya Walei
Wageni waalikwa,
Wanawake Wakatoliki wote toka majimbo yote ya Tanzania.
Mabibi na Mabwana.

Kwa Upendo wa Kristo – Tutumikie na Kuwajibika!!

Kwa heshima kubwa uongozi na Wanawake Wakatoliki Tanzania katika ujumla wetu , tunapenda kuwasilisha Risala fupi itakayoonyesha maendeleo na changamoto mbalimbali tulizokutana nazo katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake mwaka1972.

Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake kwa WAWATA katika ngazi zote, tukianzia ngazi ya Jumuiya ndogo ndogo, vigango, dekania, parokia, majimbo na hata Taifa zima kwa ujumla. Tuna kila sababu ya kumtukuza Mungu katika kipindi hiki cha miaka 40 ya uhai wa WAWATA katika Taifa letu.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Kwa namna ya pekee tunakushukuru sana kwa kukubali kwako kutufungulia Maonesho haya baada ya kuadhimisha nasi Misa ya ufunguzi hapo jana ambayo iliashiria kuanza rasmi kwa wiki ya adhimisho la Kilele cha Miaka 40 ya WAWATA .

Aidha kwa nafasi ya sherehe za Miaka 40 ya WAWATA ,tunawashukuru sana Baraza la Maaskofu ambao mwaka 1972 waliidhinisha kuanzishwa kwa Chombo Hiki na kwa uongozi wao uliosaidia sana katika kuukuza umoja huu hadi ukaenea majimbo yote ya Tanzania na kujulikana kimataifa .

Katika vipindi mbalimbali Tumekuwa na Maaskofu wengi Wenyeviti wa Idara ya Utume wa Walei pamoja na Makatibu wa Idara ya Utume wa Walei Baraza la Maaskofu wakiwemo mapadre watawa na viongozi mbalimbali.Wote wamekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya WAWATA katika ngazi mbalimbali. Pamoja na shukrani za dhati kwa hao wote WAWATA wanazidi kuwaomba ushirikiano wao katika kipindi kipya cha Upendo kwa Vitendo.

Kwa nafasi hii ya adhimisho la miaka 40 ya WAWATA na hasa kwa faida ya wageni na wale wote ambao hawana picha ya hiki chombo kimeanzia wapi, ni vema tukaelezea kwa ufupi sana WAWATA ni nini.

Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) ni chombo cha Kanisa Katoliki kilichoundwa kutokana na maazimio ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano. Baada ya azimio hili kutolewa katika Mtaguso huo, Kila nchi ilichukua na kuanza utekelezaji kadiri muda na uelewa wa azimio hilo ulivyoruhusu na kuwafikishia waamini wake.

Kwetu sisi Tanzania, umoja huu ulianza kuzama ndani ya mioyo ya watu mwaka 1972. Na nia kuu ya kuanzishwa Umoja huu, ilikuwa kutoa fursa kwa Wanawake Wakatoliki kushiriki na kushirikisha Utume wao katika Kanisa kama wanawake Wakristo kwa kutumia karama na vipaji mbalimbali walivyojaliwa na Mungu kwa nia ya kulistawisha kanisa la Kristo hapa duniani..

Taswira (vision):
Taswira ya WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanakuwa na maendeleo ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji ya familia na michango ya maendeleo ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Yesu Kristo.

Malengo:
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Umoja huu ulipoanzishwa, ulijiwekea malengo ili kupata mwelekeo utakaotufikisha mahali ambapo tunaweza kufanya tathmini ya Utume wetu katika kanisa na ukombozi mzima wa mwanamke katika suala la kiroho, ujinga, umaskini na uwezo. Malengo yalikuwa kama yafuatavyo:

    Kumjenga mwanamke katika Imani thabiti ya Kikristo, aishi maisha matakatifu, atakatifuze malimwengu.


    Kumjengea uwezo wa kujikomboa yeye na familia yake ili akomboe wengine wenye shida, yatima na wasiojiweza.


    Kumwendeleza mwanamke kielimu na kiujuzi ili aondokane na giza la kiroho, ujinga wa akili na aendeleze wengine


    Kumwezesha mwanamke katika maswala ya kiuchumi ili kutegemeza familia, kanisa na kuwategemeza wengine.


Mafanikio na Changamoto:
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,Wanawake Wakatoliki Tanzania katika kipindi cha miaka 40,Tukitathmini tulivyoanza na sasa, ni wazi kwamba tunamshukuru Mungu kwa hatua kubwa iliyofikiwa. Baadhi ya changamoto tulizokabiliana nazo ni:

    Kabla ya umoja huu kuanzishwa, kulikuwa hakuna ushirikishwaji wowote wa utume wa wanawake katika Kanisa – Leo hii wanawake wanashirikishwa katika kuinjilisha, mikutano ya kanisa, Uongozi wa kanisa na mambo mengi ya maamuzi katika kanisa.


    Umoja huu ulipoanza, mfumo wa uongozi ulianzia Taifani, na kupatikana viongozi haikuwa rahisi, katika juhudi za kuwaelimisha wanawake nafasi yao na wajibu wao katika Kanisa, uongozi uliingia katika ngazi ya majimbo, pole pole maparokiani, vigangoni na sasa uongozi umepenya mpaka kwenye jumuiya ndogo ndogo kuhakikisha kuwa Utume wa mwanamke mkatoliki katika kanisa unamfikia kila mwanamke mbatizwa katika kanisa la mahali.


    Swala la malezi ya watoto na vijana, wanawake walizoea kulelea kwenye ngazi ya familia zaidi, lakini leo hii, wanawake wameshika hatamu ya malezi kwenye Jumuiya ndogo ndogo, wanafadhili seminari zetu, vituo vya watoto yatima na vituo vingine vya malezi kwa ushirikiano mkubwa na watawa wa kike.


    Swala la maendeleo ya jamii na uchumi, wanawake walizoea zaidi kazi za nyumbani, kilimo na ufugaji lakini leo pamoja na hizo, wanawake wamejikita katika ujasiriamali mdogo na mkubwa ambao umekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na uchumi wa nchi.


Leo katika maonesho ya kazi za wanawake wakatoliki umeona juhudi walizo nazo katika majimbo yote katika nyanja zote za Utume katika kanisa na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Katika Utume wa Kanisa:

Majimbo yameonesha uwajibikaji wa matendo ya huruma, kufundisha watoto na vijana, ushiriki katika jumuiya ndogo ndogo, mafungo, hija mbalimbali, makongamano, kutembelea vituo vya yatima, magereza na wagonjwa, kutegemeza seminari zetu, kushiriki michango mbalimbali ya ujenzi wa makanisa pia kuwatia moyo vijana wetu wanaopata madaraja ya kanisa na kuwekwa wakfu kwa kuwazawadia zawadi mbalimbali, matoleo ya vipaji mbalimbali kwa ajili ya watumishi wa Mungu

Katika maendeleo na Uchumi: Majimbo yameonesha:
Mahudhurio ya vikao na mikutano ya maamuzi, uanzishwaji wa mifuko ya kuweka na kukopa, ujenzi wa vituo vya mafunzo na shule za watoto wadogo, miradi ya WAWATA kiparokia, kijimbo na kitaifa, aidha tunachukua fursa hii kuwashukuru sana wafadhili wetu wa nje ya nchi, akiwemo Mr.Viliger ambaye yupo hapa leo kwa mbegu ya ‘Revoling Fund’ waliotupatia ambayo kwa uhakika ilitupa hatua nzuri ya kuingia katika ujasiriamali. Wanawake ambao hawakuwa na jinsi ya kujikwamua katika umaskini, Mbegu hii ilikuwa ukombozi na leo hii wanawake wengi wana viwanda vyao, maduka, mashule na biashara nyinginezo kwa kupitia msaada huu. Ijapokuwa wapo walioshindwa kutembea na mfuko huu, lakini asilimia kubwa walifanikiwa na baadhi ya mafanikio umeyaona kwenye maonesho yetu.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Maendeleo ya WAWATA katika kipindi hiki cha miaka 40, si rahisi kuweza kuyaandika yote ila hatutasahau ushirikiano tulio nao na vyama vingine vya kanisa na Serikali ambavyo vimekuwa kama daraja kuu la kuwafikia wanawake wengi katika kanisa na makanisa na Taasisi mbalimbali ambazo aidha wanatupatia huduma sisi au WAWATA wanapeleka huduma.

Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo,utayari wako wa kuwa nasi katika tukio hili muhimu unatutia moyo sana moyo sana sisi WAWATA katika Utume wetu. Adhimisho hili la miaka 40 tulilizindua rasmi Mwezi Septemba 2011 .Katika kipindi hiki adhimisho hili limefanyika nchi nzima katika ngazi zote za kanisa katoliki Tanzania kwa mambo yafuatayo:

    Tafakari za Kiroho

Tafakari za kina za kiroho kuhusu kauli Mbiu ya adhimisho ambayo ni “Upendo kwa Vitendo-love in action” kauli mbiu ambayo Wanawake Wakatoliki Dunia nzima Tuliipitisha katika Adhimisho la Miaka 100 ya Umoja wa Jumuiya za Wanawake Ulimwenguni lilifanyika huko Israel mwaka 2010 .Upendo ni Mhimili wa mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristu na hakika binadamu tukiishi kwa Upendo Amani na maelewano vitajengeka. Tunashukuru sana Kwamba Balozi wa Baba Mtakatifu amekubali Kufungua rasmi Tafakari yetu ya kuhitimisha Miaka 40 siku ya Ijumaa tarehe 28/9/2012 itakayowawezesha WAWATA kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa miaka mitano ijayowa kiongozwa na kauli Mbiu y a Upendo kwa Vitendo. Aidha tunamshukuru sana Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania kwa kukubali kuadhimisha Misa ya kilele cha adhimisho letu kumshukuru Mungu na kumtukuza Somo wetu Bikira Maria Msaada wa Wakristu itakayofanyika katika kanisa kuu la Mt Yosefu siku ya Jumapili tarehe 30/9/2012.

    Hija katika sehemu Takatifu

Moja ya matukio muhimu katika sherehe za miaka 40 ya WAWATA ni Hija za WAWATA sehemu mbalimbali takatifu nchini na nje ya nchi .Ofisi ya WAWATA taifa ilifanikiwa kuratibu hija ambayo ilijumlisha maeneo matatu:Vatikano-Roma ambapo mahujaji walionana na Baba Mtakatifu benedicto wa 16, Lurdis ambako Bikira Maria alimtokea Mt.Bernadetta na Israel.Tunawapongeza WAWATA majimbo yote katik a ushiriki wao katika hija mbalimbali

    Matendo ya Huruma

Katika adhimisho hili mwaka Mzima WAWATA walifanya matendo ya Huruma kuwasaidia wasijiweza katika jamii nzima kwa hali na mali.Aidha walishiriki pia katika kufadhili seminari na vituo kadhaa vya kanisa vinavyohudumia wahitaji.

    Maonesho ya kazi ya Utume wa WAWATA

Maonesho ya kazi za utume wa WAWATA kama ulivyojionea yanaainisha kazi mbalimbali za WAWATA mathalani Miradi mbalimbali ya kumkomboa mwanamke katika umaskini, Uinjilishaji ,Ushiriki wa Mwanamke Mkatoliki katika shughuli za kijamii pamoja na Wanawake Wakatoliki wanavyoshiriki katika kulitegemeza kanisa na Taifa letu kwa ujumla.

    Ushiriki katika Kujadili katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Uongozi wa WAWATA katika adhimisho hili utapata fursa ya kujadili Katiba ya Nchi yetu ili kuwaandaa kushiriki kikamilifu fursa waliyopewa ya kushiriki mchakato huo ili katiba yenye kukidhi matakwa ya watanzania na yenye kuzingatia mpango wa Mwenyezi Mungu iweze kupatikana.

Hitimisho:
Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hayo yote aliyotujalia, tunaomba atusaidie kusiwepo na kurudi nyuma bali tusonge mbele zaidi na zaidi tukizidi kuleta mshikamano wa wanawake wakatoliki wote pia wanawake wa madhehebu ambako WAWATA ni moja katika umoja wa Wanawake wa Madhehebu ya Kikristo kitaifa na majimboni .

Kwa namna ya pekee, tunakushukuru sana Mwadhama,Balozi wa Baba Mtakatifu pamoja na Waandamizi mliofuatana nao kwa kuutoa muda wenu kwa ajili yetu siku hii ya leo, tukijua wazi kuwa mna shughuli nyingi za Kichungaji. Mwenyezi Mungu awabariki sana na kuwajalia maisha marefu yenye amani tele.

Tunawashukuru watu wote,pamoja na wageni kutoka nchi za nje, Kenya, Uganda, Malawi na Zambia, walioacha shughuli zao wakaja kuungana nasi katika tukio hili kuu la WAWATA kutimiza miaka 40. Mungu awabariki sana. Wabarikiwe pia WAWATA wote waliojitoa kwa hali na mali katika kufanikisha shughuli hii, Mungu awabariki na kuwafanikisha katika malengo yenu.

Tunawashukuru sana Waasisi wa Umoja huu pamoja na Viongozi wote waliokwisha pitia katika ngazi mbalimbali ambao leo tunasifu kazi zao na mafanikio kwa hii miaka 40. Mungu awazidishie neema zake popote walipo.

Asanteni sana

“Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika”

Wanawake Wakatoliki Tanzania










All the contents on this site are copyrighted ©.