Katekesi ya Baba Mtakatifu Benedikto XV1, kwa Jumatano hii, imeendelea na Mada ya
mwaka wa imani, na amezungumzia, namna tunavyoweza kumwasilisha Mungu katika nyakati
hizi zetu. Kuiwasilisha imani ya Kikristu kama jibu la uhakika katika matamanio yote
ya roho ya binadamu. Papa anasema, hii inamaanisha kumpeleka Mungu wa Kristu kwa
watu wote, wake kwa waume wa nyakati hizi zetu. Ni kushuhudia ujumbe wa Injili kupitia
maisha manyenyekevu kila siku. "Hii ni habari njema ya Mungu ambayo ni Upendo
, unao tuwezesha sisi kuwa karibu na Yesu Kristu hata wakati wa vipindi vigumu vya
majaribu ya Msalaba, na kwa Ufufuko wake, tunajazwa na tumaini na ahadi yake ya maisha
ya milele. Yesu ni ishara ya upendo wake, unao jali haja za maisha na mahitaji yetu,mwenye
kutuongoza kwa Baba ". Papa aliendelea kusema , katika utume huu wa kumpeleka
Mungu kwa watu wa nyakati hizi zetu, familia inakuwa ni nafasi nzuri, kupitia mfumo
wake wa kifamilia, kuiishi imani katika maisha yake ya kila siku, yaliyo jazwa na
tumaini na matazamio ya maisha ya milele, kwa furaha ya mazungumzano , msamaha na
upendo. Upendo wa Kristu ulio dhihirisha ukuu wetu kama watu waliokombolewa kwa
upendo wake na kuitwa katika Kanisa, kuujenga mji mpya wa binadamu ili kwamba uweze
kuwa ni Mji wa Mungu.