2012-11-28 10:51:03

UNHCR yaanza tena kutoa huduma kwa wakimbizi Goma, DRC


Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limeanza tena kutoa huduma kwa wakimbizi walioko kwenye kambi kumi na mbili katika eneo la Goma. Kwa sasa Shirika linaendelea kugawa chakula cha msaada kwa ajili ya wakimbizi laki moja na kumi wanaohitaji chakula cha msaada, baada ya mji wa Goma kutekwa na kushikiliwa na Kikosi cha M23.

UNHCR ina tumaini kwamba, wakimbizi wengi watapata ujasiri wa kuweza kurudi kwenye makazi yao kwani, chakula kilichopo kinaweza kutosheleza kwa siku chache tu. Umoja wa Mataifa unaendelea kuangalia hali ya usalama wa raia na mali zao, ili wananchi waweze kuruhusiwa kurudi tena kwenye makazi yao.

Hivi karibuni zaidi ya watu laki moja na arobaini, walilazimika kuyakimbia makazi yao ili kutafuta hifadhi mjini Goma baada ya machafuko ya kivita kupamba moto. Wakimbizi wengi bado wanahitaji msaada wa chakula na maji safi na salama, ili kuepuka uwezekano wa kulipuka kwa magonjwa ya kuambukiza.







All the contents on this site are copyrighted ©.