2012-11-28 08:37:00

Miaka 40 ya WAWATA, TANZANIA


Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, hivi karibuni kimeadhimisha miaka arobaini tangu kuanzishwa kwake, sherehe ambazo zilifunguliwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Majimbo Katoliki Tanzania na baadhi ya wawakilishi kutoka katika nchi ambazo ni Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. RealAudioMP3

Katika mahubiri yake, Kardinali Pengo aliwakumbusha WAWATA kwamba uwepo wao ndani ya Chama hiki cha kitume unapania kwa namna ya pekee kuwajengea uwezo wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Ni kundi ambalo linatakiwa kutangaza Injili ya Upendo wa Kristo unaowawajibisha, kama inavyobainishwa katika kauli mbiu ya WAWATA.

Maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka arobaini, ilikuwa ni fursa ya kuweza kufanya tafakari na tathmini ya kina kuhusu: malengo, utume na ushiriki wao katika maisha ya Kanisa mahalia. Ni kipindi cha kuchunguza dhamiri kwa kuangalia pale walipofanya vyema ili kuongeza juhudi zaidi na pale ambapo wamechechemea waweze kuparekebisha mapema kabla mambo hayaenda mrama. Uwepo wao ndani ya WAWATA isiwe ni nafasi ya kutaka kujijenga kisiasa, kijamii wala kiuchumi.

WAWATA kama Chama cha kitume kinapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, kwa kusimama kidete kujenga na kuimarisha Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati, daima wakijitahidi kutafuta mafao ya wengi. Wanawake Wakatoliki wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda, kudumisha na kutetea zawadi ya maisha, tangu pale mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika, kamwe wasithubutu kukumbatia utamaduni wa kifo kwani tendo hili ni kusaliti utume na dhamana yao kama Wanawake Wakatoliki.

Katika kipindi cha miaka arobaini ya uwepo wake, WAWATA imejitahidi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umaskini miongoni mwa wanawake kwa kuwajengea uwezo kiuchumi na kijamii, ili aweze kujitegemea na kuzitegemeza familia zao. Kuanzia sasa Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kuwa ni chachu ya umoja na mshikamano wa dhati, kwa kutambua kwamba, wao ni makatekista wa kwanza katika kufundisha na kurithisha imani, maadili na tunu bora za maisha ya kijamii.

Ni vyombo vya Injili ya Upendo, inayopaswa kutekelezwa si kwa maneno tu bali kwa njia ya vitendo, kwa kuwajali na kuwasaidia watoto, wazee, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kila mtu aweze kuonja upendo wa Kristo unaoendelea kuwawajibisha.

Kardinali Polycarp Pengo wakati alipokuwa anatoa hotuba yake kwenye ufunguzi wa maonesho ya bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa na Wanawake Wakatoliki Tanzania, aliwakumbusha kwa namna ya pekee, kumwilisha ndani mwao kauli mbiu inayowataka kutekeleza upendo wao kwa njia ya vitendo. Maonesho haya yalikuwa ni vielelezo vya kazi ya Mwanamke Mkatoliki katika mchakato wa kujiendeleza kiroho na kimwili; hususan katika: uchumi, malezi, utunzaji wa mazingira, mafundisho ya dini na maadili na utu wema. Huu ni mchango mkubwa wa WAWATA kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla wao.

Wanawake Wakatoliki wamekuwa mstari wa mbele kushiriki katika maisha ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu, kwani kwa njia ya Jumuiya zinazowajibika, hapo Kanisa linapata Familia bora, imara na makini zenye kutoa viongozi bora kwa Kanisa na Taifa.

Wanawake Wakatoliki wanapania anasema Kardinali Pengo kumkomboa mwanamke kutoka katika hadha mbali mbali za maisha, unyanyasaji, ujinga na maradhi, kwa kujikomboa wao wenyewe, wanakuwa pia ni vyombovya ukombozi kwa watu wengine na kuwa ni chachu ya maendeleo katika ngazi mbali mbali. Kardinali Pengo anasema, uongozi unaowajibika na kujikita katika uaminifu unapotekeleza yote haya ni muhimu sana katika mchakato mzima unaopania kuhakikisha kwamba, shughuli hizi zinakuwa ni hai na endelevu, ili kuleta mabadiliko katika Jamii kwa kusimama kidete kutafuta mafao ya wengi.

Kardinali Pengo anawahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Tanzania, kwani huu ni wajibu wa msingi kikatiba, dhamana wanaopaswa kuitekeleza kwa uaminifu mkubwa zaidi wakisukumwa na kauli mbiu upendo kwa vitendo, inayoongoza maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka arobaini tangu WAWATA ilipoanzishwa kama Chama cha Kitume na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Ni changamoto kwa WAWATA kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao, kama Kristo mwenyewe alivyofanya kwa kuhubiri, kuponya, kusamehe na kuwakirimia watu mahitaji yao. Ni jukumu lao kudumisha na kuendeleza misingi ya amani kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Jamii. Familia inapaswa kuwa ni shule ya kwanza ambamo watoto wanajifunza upendo wa dhati kutoka kwa wazazi wao, ili waeeze kuwa kweli ni raia wema.

Jukumu ambalo liko mbele yao kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi bora ya watoto na vijana, ili kulea na kustawisha amani ambayo inaendelea kuyumba siku hadi siku. Familia zioneshe upendo kwa vitendo ili Jamii iweze kuwatambua kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo.

Sherehe za ufunguzi wa maonesho ya kazi za mikono ya Wanawake Wakatoliki Tanzania zilihudhuriwa pia na Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania pamoja na viongozi mbali mbali kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Wanawake WaKatoliki Tanzania.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya kumbu kumbua ya miaka arobaini ya WAWATA, Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, aliasema, Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa mwanamke Mkataoliki katika azma ya Uinjilishaji inayojikita katika malezi, maisha ya kiroho kwa tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti, daima wakijitahidi kuiga mfano wa Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji Mpya.

Askofu Rwoma aliwataka wanawake wakatoliki kuwa na ujasiri kwa kuielewa misingi sahihi ya imani yao na hivyo kuitafsiri kwa vitendo katika medani mbali mbali za maisha, daima wakisimama kidete kutetea Injili ya uhai, wakidumisha utu na maadili mema. Anawaalika WAWATA kujikita vyema zaidi katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliozinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Wawe mstari wa mbele kuwainua wanawake wenzao kutoka katika unyonge, umaskini na dhuluma, kama sehemu ya mchakato unaopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu Rwoma anawataka WAWATA kama vilivyo vyama mbali mbali vya kitume nchini Tanzania, kujiandaa barabara kwa ajili ya kushiriki na hatimaye, kufanikisha uchaguzi mkuu wa vyama vya kitume; kwa kuzingatia kiwango cha elimu pamoja na kusoma alama za nyakati kutokana na mabadiliko makubwa yanayojionesha kwenye ulimwengu mamboleo na mwingiliano wa watu, kwani leo hii ulimwengu ni kama Kijiji.








All the contents on this site are copyrighted ©.