Maandalizi makini yanahitajika kabla ya kupokea Sakramenti za Kanisa
Mpendwa msilizaji wa Radio Vatican, karibu tena katika mfululizo wa vipindi vyetu
vya Uinjilishaji wa kina tukiendelea bado kuchambua Mwongozo wa maadhimisho ya Sinodi
ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya. Juma hili tuendelee na sehemu ya mchakato mzima
wa uinjilishaji katika kuwaingiza Watu wa Mungu katika Ukristo.
Uenezaji wa
Imani katika ulimwengu unaobadilika kila siku unaleta changamoto nyingi katika ulimwengu
wa Ukristu. Hali imepelekea katika Kanisa kuwepo kwa majadiliano ya Kina juu ya changamoto
hizo jambo ambalo limepelekea kuitishwa kwa Sinodi maalum juu ya tema hii ya Uinjilishaji
Mpya. Nyaraka zilizotolewa katika Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican sasa yametimia machoni
pa Kanisa.
Sakramenti za kuingiza watu katika Ukristo yaani: Ubatizo, Kipaimara
na Ekaristi Takatifu hivi sasa si Sakramenti tofauti tena miongoni mwa Waumini bali
zimeunganishwa na kuwa hatu kuu tatu msingi za kumwingiza mtu katika Imani ya Kikristo.
Hii ni hatua muhimu sana iliyofikiwa na Kanisa mahali ambapo Waumini wanazielewa barabara
sakramenti hizi msingi katika maisha yao.
Katika mchakato huu, bado kuna kutofautiana
katika maadhimisho ya sakramenti hizi pia kuna changamoto nyingi zitokanazo na umuhimu
wa sakramenti hizi katika Kanisa kati ya Kanisa la Magharibi na lile la Mashariki.
Pia bado kuna dukuduku hususan juu ya ubatizo wa watoto wadogo na uhuru wa mtu kuchagua
imani anayoitaka.
Tofauti hizi zinatoa mwaliko kwa Kanisa kutoa majibu ya
kufaa yanayokidhi haja ya wanafamilia ya Mungu kiulimwengu. Hivyo Kanisa linaalikwa
kufanya upya tathmini ya namna ya kumwingiza mtu Ukristo likizingatia umoja wa Kanisa
kiulimwengu. Bado pia kuna changamoto hata ya namna ya maadhimisho ya mafumbo na ibada
za Kikristu mintarafu maswala ya Liturujia na lugha ya kutumia. Kuna mvutano kati
ya wanafamilia ya Mungu ambao unahitaji tathmini na kutolea majibu ya wazi ya kiteologia,
kiimani na kimapokea.
Ulimwengu wa leo bado unaleta changamoto nyingine kwa
wanafamilia ya Mungu yaani pale wanapojitokeza watu wengine katika mijadala ya mambo
ya Mungu. Wanafamilia ya Mungu, walio wengi wanashindwa kujibu maswali katika mijadala
kama hii na kubaki kukaa kimya na kushindwa kabisa kuitetea imani yao hali ambayo
imepelekea wengi kunaswa na madhehebu mengine kwa kufikiri kuwa kule wanapata majibu
sahihi kuhusu imani yao.
Aidha, kukosekana kwa Katekesi ya kina mtu anapoingizwa
Ukristo kumepelekea kuwa na wanafamilia ya Mungu wasiokomaa kiimani na mara wanaokumbwa
na changamoto kimaisha na kiimani hubabaika na kurudi nyuma.
Hati hii imelitaka
Kanisa kubuni mbinu itakayoliwezesha Kanisa kwajenga Waamini wake kiimani na pia kimafundisho.
Utangazaji wa Neno la Mungu kwa mara ya kwanza kwa watu ambao hawajaisikia kabisa
imani lazima ufuatane na Katekesi ya kina ili kuweza kuwakomaza kiimani watoto wapya
katika Kanisa.
Katekesi mbali na utangazaji wa Neno itasaidia mchakato mzima
wa wongofu wa mtu kumwelekea Mungu. Hivyo makanisa mahalia yamealikwa kupokea mwongozo
utakaotolewa na Mababa wa Sinodi, na kuketi chini na kuona namna gani kulingana na
hali na mazingira ya Kanisa mahalia wanaweza kufanya uenezaji wa imani uzae matunda
yaliyokusudiwa.
Wakati umefika ambapo lazima Wanafamilia ya Mungu wazoee kwanza
kabisa kuongea juu ya Imani yao mbele ya watu wengine wenye mtazamo kidogo tofauti
na wao au hata kwa wenzao wenye njaa ya kutaka kujiimarisha zaidi kiimani. Tofauti
na mtindo wa zamani kidoko ambapo Wachungaji tu ndio waliotegemewa kutoa majibu juu
ya maswali ya kiimani sasa Kanisa lazima liwandae vema watoto wao kuweza kucheza kwa
uhuru na watoto wengine bila kuwa na hofu.
Kwa upande wa Wanafamilia ya Mungu
wakati umefika kufungua mioyo yao na kujikita moja kwa moja katika mchakato mzima
wa uinjilishaji kwa wao wenyewe kujibidisha kufahamu fika angalau yale ya msingi ambayo
kimsingi ndiyo yanayoulizwa na wengi mitaani.
Mpenzi msikilizaji wakati ukuta,
ukishindana nao utaumia! Hadi hapa tumefikia mwisho wa makala yetu kwa siku ya leo.
Nakutakia kila neema na Baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kutoka Studio za Radio Vatican
ni mimi mtayarishaji na msimulizi wako Padre George wa Bodyo.