2012-11-27 08:57:28

Jimbo Katoliki Mbeya linajiandaa kuadhimisha Sinodi ya Jimbo kwa kujikita katika Utume wa Familia


Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania anatarajiwa kufungua Maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, Januari, 2013 kwa kupania kujikita zaidi katika Utume wa Familia. Waamini wataweza kupata nafasi ya kutembeleana nyumba hadi nyumba ili kuimarisha Utume wa Familia, ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbali mbali kutoka ndani na nje ya familia yenyewe.

Askofu Chengula anabainisha kwamba, Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, itakuwa ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wake mintarafu mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican. Katika maadhimisho hayo, Jimbo Katoliki Mbeya, litazindua pia Mkakati wa shughuli za kichungaji, ambao utakuwa dira na mwongozo wa Jimbo Katoliki Mbeya kwa miaka kadhaa ijayo.

Kanisa linapenda kuimarisha imani miongoni mwa waamini kwa kujikita zaidi katika masuala ya Maandiko Matakatifu, Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na kuendelea kutafakari kuhusu utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; changamoto kwa waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha, sanjari na kuendeleza jitihada za Mama Kanisa katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao amini.

Maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, itakuwa ni fursa kwa Kanisa Jimboni Mbeya, kufanya tathmini ya kina kuhusu: majadiliano ya kidini na kiekumene, ikizingatiwa kwamba, Mbeya ni kati ya mikoa ambayo ina idadi kubwa ya madhehebu mbali mbali ya Kikristo, pengine, kuliko sehemu nyingine yoyote ya Tanzania. Ni muda wa kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kujenga na kuimarisha misingi ya: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; daima wajikitahidi kutafuta mafao ya wengi.

Uchumi na maendeleo ya Kijamii ni mada itakayochambuliwa mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa, ikizingatiwa kwamba, leo hii kuna idadi kubwa ya watu wanaoendelea kutumbukia katika baa la umaskini, ujinga na njaa na kwamba, hali inazidi kuwa mbaya hata kuliko ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita! Hapa kuna haja ya sera na mikakati ya maendeleo kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, Askofu Evaristo Chengula anatarajiwa kutoa Waraka mara baada ya Sinodi, utakaokuwa ni dira na mwongozo wa Kanisa Katoliki Mbeya katika mikakati yake ya shughuli za kichungaji na kitume! Ni mwaliko kwa Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mbeya kushikamana na kutembea kwa pamoja, ili waweze kwa pamoja kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.