2012-11-26 09:33:08

Mwongozo kuhusu Kanuni ya Misa kwa Lugha ya Kiswahili


Hivi karibuni yalichapwa na kusambazwa majarida kwa ajili ya Kanuni Mpya ya Misa. Majarida makubwa yalichapwa kwa ajili ya Mapadri Waadhimishi na majarida madogo yalitayarishwa kwa ajili ya Mapadri Waadhimishaji Wenza na kwa ajili ya waamini kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya ibada ya Misa.
Tunaomba radhi kwa usumbufu, kumeonekana makosa ya uchapaji na tafsiri katika majarida makubwa. Kwa hivi kumefanyika marekebisho katika majarida makubwa na Idara ya Liturujia TEC imeamua kuchapa upya majarida hayo kwa ajili ya Mapadri Waadhimishi.
Uchapaji unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Majimbo ambayo yalishanunua majarida makubwa, yatapelekewa majarida mapya bila malipo mengine. Majimbo mengine yaendelee kuagiza majarida mapya kwa bei ile ile ya fedha za kitanzania shilingi 3,000 tu kwa kila jarida kupitia anwani hii:

TMP BOOK DEPARTMENT TABORA
P.O.BOX 550 TABORA
TANZANIA
Tel. 0265097 / 026 2604244
e-mail: tmpbookdept@yahoo.com

Majarida madogo yaliyotayarishwa kwa ajili ya Mapadri Waadhimishi Wenza na Waamini yanaweza kutumika. Hata hivyo, tumeamua kuchapa upya majarida hayo ili yaweze kuwa na maandishi yanayosomeka kirahisi zaidi na tena kupunguza ukubwa wake ili iwe rahisi kushikika. Bei yake itatangazwa baadaye.

Tunawakumbusha waamini wote kuwa kadiri ya Kanuni Mpya ya Misa viitikizano vya Misa vimebadilika. Mfano:

Kiongozi wa ibada anaposalimia: Bwana awe nanyi,
Wote wanaitikia: Na awe rohoni mwako.

Katika gazeti la Kiongozi la ijumaa tarehe 16/11/2012 na ijumaa tarehe 23/11/2012 maelezo yametolewa kuhusu sababu za mabadiliko haya. Kwa kifupi tafsiri mpya ya Misale ya Altare inazingatia Misale ya Altare ya kilatini:
Mf. Dominus vobiscum: Et cum spiritu tuo, maana yake Bwana awe nanyi: Na awe rohoni mwako.

Kanuni Mpya ya Misa itaanza kutumika rasmi katika kanisa letu hapa Tanzania kuanzia tarehe 02. 12.2012 Jumapili ya kwanza ya Majilio.

Tunapenda kukumbusha pia muagize KALENDA YA LITURUJIA zinazotengenezwa na Baraza la Maaskofu ambazo pia zi tayari. Ni muhimu sana kuagiza kalenda zetu ili: kujua kwa undani maana na namna ya kuadhimisha mafumbo mbali mbali katika mwaka wa kanisa, kujua matukio muhimu katika majimbo yetu, kwa mfano, tarehe za kutabarukiwa makanisa ya jimbo, za kupata daraja ya uaskofu, kumbukumbu ambazo zimeombewa hadhi ya kuwa sikukuu katika nchi yetu, n.k.

TUNAWATAKIA USHIRIKI HAI KATIKA MAADHIMISHO YA IBADA YA MISA

Padri Paterni Patrick Mangi
Katibu Mtendaji
Idara ya Liturujia, TEC.








All the contents on this site are copyrighted ©.