2012-11-26 13:30:13

Mkutano wa Kimataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi wafunguliwa mjini Doha, Qatar


Wajumbe kutoka nchi mbali mbali wanakutanika mjini Doha, Qatar, kujadili kwa mara nyingine tena, mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani kwa kuziwezesha Nchi zinazoendelea kukabiliana na majanga haya ambayo yameendelea kuwa ni sababu ya umaskini kwa watu wengi duniani. Katika kipindi cha miaka zaidi ya kumi, Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikijadili mikakati ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi lakini bila mafanikio.

Juhudi hizi ziligonga mwamba wakati wa mkutano wa Copenhagen, miaka mitatu iliyopita, wakagonga mwamba tena mwaka 2011, sasa wamejipanga ili kuweza kufikia muafaka ifikapo mwaka 2015.

Mambo kadhaa yanapaswa kupatiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na kujipanga kubeba gharama kubwa ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kati ya nchi tajiri duniani na nchi maskini. Wajumbe wanaangalia pia uwezekano wa kurefusha Itifaki ya Kyoto, kwa ajili ya nchi tajiri zaidi duniani sanjari na kutafuta fedha zitakazotumika kwenye nchi changa duniani, kama njia ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, dunia inakuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi hata kwa siku za usoni. Wanaharakati na watunza mazingira wanabainisha kwamba, mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu mikakati ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi yanakwenda mwendo wa "Kinyonga".

Mkutano wa mabadiliko wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi umefunguliwa Jumatatu, tarehe 26 Novemba 2012. Mafuriko, vimbunga, ukame wa kutisha ni kati ya mambo ambayo yatakuwa na athari kubwa katika maisha ya watu na harakati za maendeleo kwa ujumla, kama inavyojionesha katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya wanaounda asilimia kumi na tano ya wazalishaji wakubwa wa hewa ya ukaa, wanaonekana kuunga mkono wazo la kuendeleza Itifaki ya Kyoto. Marekani ilipinga Itifaki ya Kyoto, kwa vile China na India ambao pia ni wazalishaji wakuu wa hewa ya ukaa hawakuwekewa masharti yoyote. Wao wanataka majadiliano kuhusu uthibiti wa hewa ya ukaa yawe katika ngazi sawa sawa, ili kuweza kupitisha Itifaki mpya.

China na India inashikilia msimamo wake kwamba, tatizo la uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo inatishia maisha na usalama wa dunia ni matokeo ya uzalishaji mkubwa viwandani unaofanywa na Marekani pamoja na nchi mbali mbali za Bara la Ulaya. Nchi hizi zinaomba kuruhusiwa kuendelea kuzalisha hewa ya ukaa kwani ndiyo zinaanza kuchipukia katika masuala ya maendeleo sanjari na kupania kuwainua watu wengi kutoka katika baa la umaskini.







All the contents on this site are copyrighted ©.