Kazi inapata chimbuko lake ndani ya Familia na ni kwa ajili ya Familia
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena tuendelee na tafakari yetu ya kazi
na familia. Na kwa namna ya pekee leo tukumbushane kuwa kazi ni kwa ajili ya manufaa
ya familia. Lakini, pia kazi inapata chimbuko lake katika familia. Kila mmoja anajua
kuwa kazi ni kwa ajili ya familia kwani kila mtu anayefanya kazi analengo la kuiwezesha
familia yake kufurahia matunda ya hiyo kazi yake. Wazazi wanapofanya kazi na hasa
ya malezi wana lengo la kufurahia makuzi na baadaye ya watoto wao. Hapa ni vizuri
tukumbushane kuwa, endapo mmoja wa wanafamilia hatatimiza majukumu yake vizuri basi
familia hiyo itaendelea kuwa na mapungufu mengi ya kimalezi, kijamii, kimahusiano
au hata kiuchumi. Lakini pia kazi ina chimbuko lake katika familia kwani kazi ni
wito au wajibu ambao mwanadamu ameupokea toka kwa Mungu. Hivyo mwanadamu anapofanya
kazi anajibu wito alioupokea toka kwa Mungu lakini kwa ajili ya ujenzi wa jumuiya
ya watu na familia ikiwa ndiyo jumuiya ya kwanza. Mwanadamu hapaswi kufanya kazi
tu kwa ajili ya faida yake binafsi bali akiwa anafahamu fika kuwa amekabithiwa jumuiya
inayomuhitaji ashirikishe vipaji vyake hivyo kutushirikisha vipaji vyake kwa ajili
ya jumuiya hii ni kuikosea haki. Ni vizuri tukumbushane kuwa kazi ambayo chimbuko
lake ni familia na kwa ajili ya familia haiishii kwenye familia tu, bali, inapanuka
na kuigusa jamii nzima. Inagusa pia mfumo mzima wa uchumi. Ndio sababu uchumi ulio
imara lazima uwe na mlingano sahihi na maisha ya jamii nzima na sio mwanadamu kugeuzwa
kuwa chombo cha ukandamizaji na uzalishaji usio na faida kwake. Kipimo cha mfumo wa
uchumi kisitegemee tu soko bali bali mahusiano ya kibinadamu aliyeko kwenye mazingira
fulani, mwenye utamaduni, lugha na historia fulani. Mwanadamu mwenye vionjo na
anayeguswa na matukio ya maisha kama ya furaha na uchungu. Kwa wakati wote tutambue
kuwa kazi, uchumi na mahusiano ya kibinadamu havitenganishwi. Tunapovitenganisha tuna
kataa ukweli kuwa kazi imetokana na mwanadamu na ni kwa ajili ya mwanadamu na si vinginevyo. Kutoka
Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphael Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi
ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.